Simba SC

BARKER AWEKA DAU KWA MPANZU KATIKA MFUMO MPYA WA SIMBA

Vardo May 28, 2026 4:20 pm

KIUNGO mshambuliaji wa Simba SC, Elia Mpanzu, ameanza kupewa jukumu jipya ndani ya kikosi hicho baada ya kocha mkuu, Steve Barker, kuamua kumbadilisha nafasi kutoka pembeni na kumtumia kama mshambuliaji wa kati.

Mabadiliko hayo yameonekana wazi katika michezo mitatu ya hivi karibuni ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo Mpanzu ameonekana akicheza zaidi katikati ya ushambuliaji huku Seleman Mwalimu akibaki benchi. Hatua hiyo inaashiria mabadiliko ya kimfumo ndani ya kikosi cha Simba kuelekea mwisho wa msimu.

Mpango huo ulianza kuonekana rasmi Mei 24, 2026, katika mchezo ambao Simba waliibuka na ushindi dhidi ya Wekundu wa Msimbazi. Katika mchezo huo, Mpanzu aliingia uwanjani akiwa na jukumu tofauti na lile alilozoeleka, akicheza kama mshambuliaji wa kati badala ya kutokea pembeni kama ilivyokuwa awali.

Akizungumzia mabadiliko hayo, Barker amesema kuwa uamuzi wa kumbadilisha Mpanzu nafasi umefanywa kwa makusudi, akiamini kuwa mchezaji huyo ana uwezo mkubwa zaidi wa kuisaidia timu akiwa karibu na eneo la hatari.

Kocha huyo amesema kwa sasa Mpanzu ni sehemu ya washambuliaji wake wa kati, huku akisisitiza kuwa mfumo huo mpya unalenga kupata matokeo bora zaidi kutoka kwa mchezaji huyo pamoja na kuifanya Simba kuwa hatari zaidi katika safu ya ushambuliaji.

“Mpanzu ni mmoja wa washambuliaji wetu kwa sasa. Nakubaliana na wewe kwamba alikuwa anatumika kuna wakati akitokea pembeni, lakini sasa atakuwa anacheza hapo. Kuna kitu bora zaidi tunakilenga kutoka kwake,” amesema Barker.

Barker ameeleza kuwa anahitaji safu yake ya ushambuliaji kuwa na kasi kubwa zaidi, ili timu iweze kutumia haraka makosa ya wapinzani mara wanapopoteza mpira kabla hawajajipanga upya kujilinda.

“Tunahitaji watu wenye kasi zaidi kule mbele. Wakati timu pinzani ikipoteza mpira, tunatakiwa kuwa na kasi ya haraka kuwashambulia kabla hawajipanga, na hilo limekuwa linafanyika vizuri,” ameongeza kocha huyo.

Mabadiliko hayo yanaonyesha wazi dhamira ya Barker ya kuifanya Simba kuwa timu yenye mchezo wa kasi na mashambulizi ya moja kwa moja, huku Mpanzu akionekana kuwa silaha muhimu katika mfumo huo mpya wa ushambuliaji.

KUHUSU HAT-TRICK KWA OKELLO…KOCHA YANGA AMTILIA NGUMU…”TIMU KWANZA”… HATMA YA IBENGE YAZUA MTIKISIKO AZAM FC