Habari za Yanga leo
Yanga SC

KUHUSU HAT-TRICK KWA OKELLO…KOCHA YANGA AMTILIA NGUMU…”TIMU KWANZA”…

admin May 28, 2026 2:21 pm

MASHABIKI wa Yanga wana furaha kuona chama lao likiendelea kushinda mechi zake za Ligi Kuu Bara na kutanua kileleni mwa msimamo, lakini anapofunga kiungo wa timu hiyo, Allan Okello basi kuna kitu wanakitamani zaidi kutoka kwake ambacho ni hat-trick, sasa kocha wa muda wa timu hiyo, Abdihamid Moallin ametoa msimamo wake akionesha kumlinda na majeraha.

Okello katika mechi dhidi ya Namungo iliyochezwa Mei 25, 2026 pale Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, alipiga bao mbili wakati Yanga ikishinda 3-1 ukiwa ni ushindi wa 18 Ligi Kuu Bara msimu huu kati ya mechi 25 ilizocheza, huku raia huyo wa Uganda akifikisha mabao 11, matatu nyuma ya kinara Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam.

Wakati Okello akifunga bao la pili dakika ya 53, mashabiki wa Yanga walitamani kuona kiungo huyo akiitafuta hat-trick kwa kufunga bao la tatu, ambayo ingekuwa ya kwanza msimu huu lakini, akatolewa dakika ya 85, nafasi yake akiingia Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Akizungumzia hilo, Moallin amesema wanatambua kiu hiyo ya mashabiki lakini kwa sasa kuna haja ya kuangalia mafanikio ya jumla ya timu na sio rekodi binafsi katika mechi zilizosalia.

Moallin amesema walilazimika kumtoa Okello ikiwa ni kumlinda asiumie wakati huu ambao wanamkosa Pacome Zouzoua aliyeumia goti kwenye mchezo wa nyuma dhidi ya Singida Black Stars ambao Yanga ilishinda kwa mabao 3-0.

“Nikweli najua mashabiki wanatamani hilo, lakini kwa sasa timu yetu lazima tuwe makini, tumemkosa Pacome (Zoouzoua) baada ya kuumia kwenye mchezo dhidi ya Singida, wote tunafahamu umuhimu wa kuwa na Pacome kwenye timu yetu,” amesema Moallin.

“Hatuwezi kufanya kosa lingine kwa kuruhusu kuumia kwa Okello wakati ambao ameshatekeleza vizuri lengo kuu la timu kushinda, tulichotakiwa ni kuulinda ushindi wetu, tuna sababu ya kuangalia mbele zaidi.

“Hatuzuii wachezaji kuweka rekodi binafsi, ikitokea wamefanya hivyo wote tutafurahia lakini kitu muhimu hapa kwetu kwasasa ni kuangalia mafanikio ya timu kwa ujumla ambayo ni kushinda ubingwa msimu huu.”

Aidha Moallin amesema ndani ya mapumziko ya takribani wiki mbili ambapo ligi itasimama kabla ya mchezo wa ugenini dhidi ya Mashujaa, Juni 13 mwaka huu, wanaamini kutakuwa na habari njema za kurejea kwa Pacome ambaye alishaanza kupatiwa matibabu.

“Pacome atarejea kwa wakati, alishaanza matibabu ya eneo ambalo ameumia, tunatarajia atakuwa tayari kabla ya kwenda kucheza mchezo unaofuata ugenini, pia nadhani kuna wengine nao watakuwa wamekaa sawa,” amesema.

SIMBA YAMTIBULIA AZAM USINGIZI KWA BEKI MZAWA BARKER AWEKA DAU KWA MPANZU KATIKA MFUMO MPYA WA SIMBA