SIMBA YAMTIBULIA AZAM USINGIZI KWA BEKI MZAWA
WAKATI mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara zikiendelea kushika kasi, vita nyingine ya kimyakimya imeanza kupamba moto nje ya uwanja kati ya Simba SC na Azam FC kuhusu kuwania saini ya beki wa kushoto, Nathaniel Chilambo.
Taarifa kutoka ndani ya vilabu hivyo zinaeleza kuwa Chilambo, ambaye mkataba wake na Azam FC unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu wa 2025/2026, ameanza kuvutia kwa kiwango kikubwa mabosi wa Simba wanaotaka kuongeza nguvu katika kikosi chao kuelekea msimu ujao.
Inaelezwa kuwa Simba imeweka kipaumbele katika kuimarisha nafasi ya beki wa kushoto, huku ikitafuta mbadala wa muda mrefu wa Shomari Kapombe ambaye kwa miaka mingi amekuwa tegemeo kubwa tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Azam FC mwaka 2017.
Licha ya uwepo wa David Kameta ‘Duchu’, mabosi wa Simba bado wanaonekana kutoridhishwa kabisa na ushindani uliopo katika eneo hilo, jambo ambalo limeifanya klabu hiyo kuhamishia macho yao kwa Chilambo kutokana na kiwango kizuri alichoendelea kuonyesha akiwa Azam FC.
Chilambo, aliyesajiliwa na Azam FC mwaka 2022 akitokea Ruvu Shooting, amekuwa akipambana kupata nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza kutokana na ushindani mkubwa uliopo ndani ya timu hiyo, ambapo Lusajo Mwaikenda ameendelea kupewa nafasi kubwa zaidi katika kikosi cha kwanza.
Hata hivyo, pamoja na Simba kuonyesha nia ya dhati ya kumpata beki huyo, Azam FC nayo imeanza hatua za mwisho za kuhakikisha inambakiza ndani ya kikosi hicho kwa kumpa ofa mpya ya mkataba wenye maslahi bora zaidi ili kuzuia kuondoka kwake.
Habari za ndani zinaeleza kuwa tayari kumekuwa na mazungumzo ya awali kati ya upande wa Chilambo na Simba SC, ingawa hadi sasa hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa. Huku dirisha la usajili likizidi kusogea, ushindani wa kuwania saini ya beki huyo unaendelea kupamba moto.