HAWA YANGA KWA FADLU WAKO SIRIAZI KWELI..?
YANGA inaendelea na msako wa kutafuta kocha mpya na sasa kuna majina mengine mawili yanatajwa akiwemo kocha wa zamani wa Simba ambaye aliibadilisha timu hiyo kurudi kwenye ubora ilionao hivi sasa.
Si unamkumbuka Fadlu Davids ambaye msimu uliopita alifanya kazi kubwa ya kuibadilisha Simba na kutisha hadi kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, basi kocha huyo wasifu wake umepitiwa na mabosi wa Yanga kisha akapigiwa simu moja juu ya kuangalia uwezekano wa kumchukua.
Hii ni mara ya pili kwa Yanga kumuhitaji raia huyo wa Afrika Kusini na awali ilimfuata wakati ikitafuta kocha mwishoni mwa msimu uliopita kipindi anaifundisha Simba, ilipomkosa, ikamuajiri Romain Folz ambaye hata hivyo waliachana naye mapema tu baada ya kuiongoza timu katika mechi sita.
Fadlu mwenye umri wa miaka 45, kwasasa anaifundisha Raja Athletic ya Morocco ambayo inautafuta sana ubingwa wa nchi hiyo na kama ataukosa, lolote linaweza kutokea katika ajira yake kutokana na presha ya mashabiki na hata viongozi wa klabu hiyo.
Taarifa zilizopo zinadai kwamba, mabosi wa juu wa Yanga wanatamani kupata kocha kijana ambaye anajua kuendeleza ubora wa wachezaji na wameona Fadlu ni mmoja kati ya wanaojua kufanya kazi hiyo.
“Tunapitia majina mengi, unajua hata Fadlu tumeongea naye, ni kocha ambaye ana vitu ambavyo tunavitaka hasa juu ya kuendeleza ubora wa wachezaji, unajua wakati akiwa Simba sisi Yanga ndio tulimharibia kutokabna na kumfunga mechi zote mbili.
“Ni kocha kijana ambaye anajua sana kazi yake na ana jicho la kutafuta wachezaji bora, sisi tunajua yupo kwenye timu anayolipwa fedha nyingi lakini kuna presha kubwa sana kushinda hii ya klabu zetu hapa,” amesema bosi huyo.
Fadlu kabla ya kutimka Simba mwanzoni mwa msimu huu akiiongoza timu hiyo katika mechi mbili akianza na kichapo cha 1-0 kwenye Ngao ya Jamii, kisha kupata ushindi wa 1-0 Ligi ya Mabingwa Afrika, msimu uliopita aliukosa ubingwa wa ligi kwa tofauti ya pointi nne uliobebwa na Yanga, lakini akaipeleka timu hiyo kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, akipoteza mbele ya RS Berkane kwa jumla ya mabao 3-1.
Mbali na Fadlu ambaye ni raia wa Afrika Kusini, Yanga pia imezungumza na kocha Amine El Karma aliyewahi kuinoa RS Berkane ya Morocco.
El Karma ambaye alipita Berkane kuanzia Novemba 11, 2022 na kuondoka Februari 11,2024, aliacha alama kwa Wamorocco wenzake hao alipowapa Kombe la Morocco msimu wa 2022-2023.
Kocha huyo aliyezaliwa miaka 40 iliyopita, hatakuwa na tabu kama akitua Yanga na anapenda kutumia mfumo wa 4-2-3-1 ambao umewahi kutumiwa na makocha tofauti ndani ya klabu hiyo.
Kabla ya makocha hao, Yanga pia imezungumza na Khalil Ben Youssef ambaye msimu huu amemaliza mkataba ndani ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini akiwa kocha wa muda, huku klabu hiyo ikitangaza kuondoka kwake kufuatia kudumu kikosini hapo kwa miaka miwili. Kocha huyo amewahi kuifundisha Yanga akiwa msaidizi wa Nasreddine Nabi wote kutoka Tunisia. Pia wote wakatua Kaizer.
Yanga ilimvutia waya Ben Youssef na kuzungumza naye ikitaka kumrudisha kikosini hapo ambapo awali hakukaa sana kwani alikuja miezi michache wakati timu hiyo ikiwa kwenye mechi za Kombe la Shirikisho Afrika kuanzia hatua ya robo fainali 2022-2023, msimu ambao ilikwenda kucheza fainali.
Bosi mmoja wa Yanga amesema zoezi la kutafuta kocha halihitaji uharaka kwani wanafanya mambo kwa utulivu wa hali ya juu kumchagua atakayekuwa bora zaidi, ndiyo maana wamekuwa wakiwasiliana na wale wanaoona wanaweza kuingia kwenye falsafa yao huku kigezo kikuu kikiwa umri na uwezo wa kuinua vipaji vya nyota wao kikosini hapo.
Ben Youssef aliyezaliwa Novemba 21, 1988, kwa sasa ana umri wa miaka 37. Kwa upande wa El Karma, amezaliwa Aprili 8, 1986 na ana umri wa miaka 40, huku Fadlu akizaliwa Mei 21, 1981, ana miaka 45. Wakati msako huo wa kocha ukiendelea, aliyeondoka Pedro Soares Gonçalves alikuwa na miaka 50, kabla ya hapo, mtangulizi wake Folz alikuwa na miaka 35.
Kwa sasa kikosi cha Yanga kinaongozwa na Abdihamid Moallin mwenye umri wa miaka 36, akisaidiana na Patrick Mabedi aliye na miaka 52.