CHAMA AWATULIZA MASHABIKI WA SIMBA, AREJEA MAZOEZINI
WAKATI hofu ikiendelea kutanda miongoni mwa mashabiki wa Simba kuhusu hali ya kiungo wao mahiri, Clatous Chama, nyota huyo ameondoa sintofahamu baada ya kurejea mazoezini na kuungana na wenzake katika Uwanja wa Mo Simba Arena.
Chama alikuwa gumzo baada ya kuonekana akichechemea wakati akitoka uwanjani katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji FC, hali iliyozua wasiwasi kwa mashabiki waliokuwa na hofu ya kumkosa katika mechi muhimu zilizobaki msimu huu.
Hata hivyo, kurejea kwake mazoezini kumetoa nafuu kubwa kwa benchi la ufundi pamoja na mashabiki wa klabu hiyo ambao wanaendelea kuamini mchango wake unaweza kuwa muhimu katika harakati za kusaka mataji yaliyosalia.
Akizungumzia hali ya kikosi, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema wachezaji wote ambao hawapo kwenye majukumu ya timu zao za taifa wameanza rasmi maandalizi ya mechi zilizosalia.
Ahmed amesema kikosi kilirejea mazoezini jana kwa lengo la kuanza maandalizi maalumu ya ratiba ngumu iliyobaki kabla ya kumalizika kwa msimu wa mashindano.
“Leo kikosi cha Simba kimerejea katika uwanja wa mazoezi kwa ajili ya kuanza programu ya michezo saba iliyosalia,” amesema Ahmed Ally.
Amongeza kuwa kati ya michezo hiyo, mitano ni ya Ligi Kuu Tanzania Bara huku mingine miwili ikiwa ya Kombe la Shirikisho la CRDB katika hatua ya nusu fainali na fainali, akisisitiza kuwa klabu hiyo inaamini ina uwezo wa kutwaa taji hilo mwishoni mwa msimu.