Simba SC

KAULI YA MAGORI YAWASHA MOTO WA UBINGWA TUNANGOJA WATELEZE

Vardo June 1, 2026 11:03 am

KLABU ya Simba SC imesisitiza umuhimu wa kuhakikisha mechi zilizobaki za Ligi Kuu ya NBC zinachezwa kwa haki na usawa, huku ikipeperusha bendera ya matumaini ya kutwaa ubingwa wa ligi pamoja na Kombe la CRDB msimu huu.

Akizungumza kuhusu hatua ya mwisho ya msimu, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori, amesema klabu hiyo inaomba kuwepo kwa usawa katika ratiba za mechi na matumizi ya viwanja ili kutoa nafasi kwa ushindani wa haki.

Kwa sasa Simba ina pointi 58 na ipo nyuma ya watani wao wa jadi, Yanga, kwa tofauti ya pointi mbili. Wekundu wa Msimbazi wanaendelea kupambana kumaliza ukame wa ubingwa wa ligi uliodumu tangu msimu wa 2020/21.

Magori amesema lengo la Simba ni kupigania mataji yote yaliyosalia, lakini akasisitiza kuwa kilicho muhimu zaidi ni kuona ushindani unafanyika kwa misingi ya haki.

“Malengo yetu ni kuwania vikombe vyote. Mechi zilizobaki ni ngumu na zina ushindani mkubwa, lakini tunachoomba ni haki. Mechi zichezwe kwa kufuata kanuni na timu iliyo bora ndiyo ishinde,” amesema.

Aidha, amewataka mashabiki wa Simba kuendelea kuiunga mkono timu hiyo katika kipindi hiki muhimu cha msimu, akieleza kuwa sapoti yao inaweza kuwa chachu ya mafanikio.

“Tumejiandaa vizuri na tunaomba sapoti ya mashabiki popote Simba inapocheza. Sina mashaka na mashabiki wa mikoani ambao wamekuwa wakijitokeza kwa wingi. Naomba pia mashabiki wa Dar es Salaam wajitokeze kwa wingi zaidi kuisapoti timu yao,” ameongeza.

Hata hivyo, Magori amekiri kuwa hatima ya ubingwa haipo mikononi mwa Simba pekee kwa sasa, kwani hata ikishinda mechi zake zote zilizobaki, bado itategemea matokeo ya mpinzani wake wa karibu.

“Ubingwa kwa sasa hauko mikononi mwetu. Tunaweza kushinda mechi zote zilizobaki, lakini kama mwenzetu atashinda zote, bado hatutakuwa mabingwa. Hii ni ligi ya marathon na chochote kinaweza kutokea katika mechi zilizobaki,” amesema.

Ameongeza kuwa Simba inaendelea kuamini kuwa ushindani bado uko wazi, huku ikipewa matumaini na uwezekano wa wapinzani wao kupoteza pointi katika hatua za mwisho za msimu.

“Tunaomba mwenzetu ateleze na sisi tushinde mechi zetu ili tuweze kutwaa ubingwa. Tunaamini pia kulikuwa na baadhi ya mechi ambazo maamuzi hayakuwa sahihi na zikatugharimu pointi muhimu ambazo pengine zingetufanya tuwe tunaongoza ligi kwa sasa,” amesema.

Pamoja na hayo, Magori alisema Simba inatambua kuwa makosa ya kibinadamu ni sehemu ya mchezo na tayari imeanza kupanga mikakati ya kuimarisha kikosi chake baada ya msimu kumalizika.

“Kutokushinda ubingwa kwa miaka minne kumetuumiza sana. Ndiyo maana tumeendelea kufanya maboresho ya kikosi na kusajili wachezaji bora ili kuongeza ushindani ndani ya timu,” amesema

Katika hatua nyingine, Magori amefichua kuwa viongozi wa Simba wamekuwa wakifanya mazungumzo na bodi ya ligi kuhusu baadhi ya masuala wanayoamini yanahitaji maboresho kuelekea msimu ujao.

“Tumekaa na viongozi wa ligi na tunaamini kuna mambo yanapaswa kufanyiwa kazi zaidi. Tunahitaji mazingira yatakayowezesha ushindani wa haki kwa kila timu ili kuongeza ubora wa ligi yetu,” amesema.

FORTUNE FARM NI SEHEMU AMBAPO BAHATI INAONGEA YANGA YAPANGA MAPINDUZI NYOTA 7 WA KIGENI KUTUA JANGWANI