Yanga SC

YANGA YAPANGA MAPINDUZI NYOTA 7 WA KIGENI KUTUA JANGWANI

Vardo June 1, 2026 11:19 am

UONGOZI wa Yanga umeanza rasmi maandalizi ya kuijenga upya timu kuelekea msimu ujao, huku ukielezwa kuwa katika mchakato wa kusaka nyota sita hadi saba wa kigeni watakaoongeza ushindani ndani ya kikosi hicho.

Hatua hiyo imekuja baada ya tathmini ya kina ya mwenendo wa timu msimu huu, ambapo baadhi ya maeneo yalionekana kuhitaji maboresho ili kuifanya Yanga kuwa na kikosi kipana na chenye uwezo mkubwa wa kushindana katika mashindano ya ndani na kimataifa.

Taarifa kutoka ndani ya klabu zinaeleza kuwa viongozi wa Yanga wamebaini kuwa baadhi ya usajili wa kigeni uliofanyika msimu huu haukutoa matokeo yaliyotarajiwa, jambo lililochangia timu kukosa wigo mpana wa chaguo katika baadhi ya nafasi muhimu.

Kutokana na hali hiyo, mabingwa hao wa Ligi Kuu wameingia sokoni mapema kwa lengo la kusaka wachezaji watakaoongeza ubora, ushindani na nguvu mpya ndani ya kikosi cha kocha kinachojiandaa na changamoto za msimu mpya.

Chanzo cha kuaminika ndani ya klabu kimeeleza kuwa Rais wa Yanga, Hersi Said, tayari ameanza kusimamia mchakato wa usajili kwa kushirikiana na benchi la ufundi ili kuhakikisha timu inapata wachezaji wanaokidhi mahitaji halisi ya kikosi.

“Rais wa Yanga, Hersi Said, ameshaanza mchakato wa usajili kwa ajili ya kuimarisha kikosi. Msimu ujao kutakuwa na mabadiliko makubwa kwa upande wa wachezaji wa kigeni,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa idadi ya nyota wa kigeni watakaosajiliwa inaweza kufikia sita hadi saba, kulingana na mapendekezo ya benchi la ufundi, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona sura mpya zitakazotua Jangwani katika dirisha kubwa la usajili.

KAULI YA MAGORI YAWASHA MOTO WA UBINGWA TUNANGOJA WATELEZE CHAMA AWATULIZA MASHABIKI WA SIMBA, AREJEA MAZOEZINI