Simba SC

MVP WA UGANDA AINGIA KWENYE RADA ZA SIMBA

Vardo June 2, 2026 10:38 am

KATIKA kuhakikisha Simba inakuwa na kikosi imara na chenye ushindani mkubwa msimu ujao, Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo imeendelea kuonyesha dhamira ya kuimarisha timu kwa kuanza kumfuatilia kiungo mshambuliaji wa Vipers SC ya Uganda, Abdulkariim Watambala, ambaye amekuwa katika kiwango bora msimu huu.

Nyota huyo amejizolea sifa kubwa nchini Uganda baada ya kuiongoza Vipers SC kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uganda msimu wa 2025/26, huku kiwango chake bora kikimuwezesha kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu (MVP).

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Uganda, Simba imekuwa ikimfuatilia kwa karibu Watambala kama sehemu ya mkakati wake wa kuongeza ubora katika safu ya kiungo mshambuliaji kuelekea msimu mpya wa mashindano ya ndani na yale ya kimataifa.

Inaelezwa kuwa viongozi wa Simba wanamuona mchezaji huyo kama chaguo sahihi la kuongeza ushindani kikosini, hasa katika kipindi ambacho hatma ya baadhi ya nyota wa kigeni ndani ya timu hiyo bado haijajulikana.

Miongoni mwa sababu zinazomfanya Watambala kuwa kwenye rada za Simba ni uwezo wake mkubwa wa kufunga na kutengeneza mabao, jambo ambalo limekuwa silaha muhimu kwa Vipers katika safari yao ya kutwaa ubingwa wa ligi.

Takwimu zinaonyesha kuwa katika mechi 28 za ligi msimu uliopita, Watambala alihusika moja kwa moja katika mabao 16, akifunga mabao 12 na kutoa asisti nne.

Rekodi hiyo ndiyo iliyompa nafasi ya kutwaa tuzo ya MVP na kuibua mvuto kutoka kwa klabu mbalimbali ndani na nje ya Uganda.

Akizungumzia mipango ya usajili, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori, amesema maboresho ya kikosi yatafanyika kulingana na mahitaji ya timu pamoja na mapendekezo ya benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Steve Barker.

“Kuna maboresho yanaendelea kufanyika kwa ajili ya kuijenga Simba bora zaidi kwa msimu ujao. Kuna wachezaji ambao tayari kocha amewapendekeza, lakini pia kuna wengine ambao tumekuwa tukiwafuatilia kwa karibu kabla ya kufanya maamuzi,” amesema Magori.

STRAIKA WA MABAO 20 AWAVUTIA YANGA, DILI LAAZA KUPIKWA MITEGO MITATU YA MWISHO YAITIKISA YANGA KUELEKEA UBINGWA