Yanga SC

STRAIKA WA MABAO 20 AWAVUTIA YANGA, DILI LAAZA KUPIKWA

Vardo June 2, 2026 10:35 am

UONGOZI wa Yanga chini ya Rais wake, Hersi Said, umeendelea kuweka mikakati ya kuimarisha kikosi kuelekea msimu ujao, huku ukiibuka mpango wa kumfuatilia mshambuliaji wa kimataifa wa Kenya, Moses Shumah, anayekipiga katika klabu ya Power Dynamos ya Zambia.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa Yanga imeanza kufanya tathmini ya kina ya uwezo wa straika huyo baada ya kuonyesha kiwango bora msimu huu na kujitambulisha kama mmoja wa washambuliaji hatari zaidi katika Ligi Kuu ya Zambia.

Shumah amekuwa akivutia macho ya wengi kutokana na makali yake mbele ya lango, akimaliza msimu akiwa amefunga mabao 20. Rekodi hiyo imeongeza hamasa kwa Yanga ambayo inaendelea kutafuta mbadala na nyongeza ya nguvu katika safu yake ya ushambuliaji.

Inaelezwa kuwa viongozi wa mabingwa hao wa Tanzania tayari wameanzisha mawasiliano ya awali ili kujua uwezekano wa kumpata nyota huyo, ingawa hadi sasa hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa kati ya pande zinazohusika.

Mbali na uwezo wake wa kutikisa nyavu, Shumah ameonyesha ubora mkubwa katika kasi, nguvu na uwezo wa kucheza chini ya presha, sifa ambazo zinaonekana kuendana na mahitaji ya benchi la ufundi la Yanga katika kuelekea msimu mpya.

Endapo usajili huo utakamilika, utakuwa sehemu ya mpango mpana wa Yanga wa kuimarisha kikosi chake kwa lengo la kuendelea kutawala mashindano ya ndani na kufanya vizuri zaidi katika michuano ya kimataifa.

 

Hata hivyo, bado ni mapema kujua hatima ya dili hilo, huku mashabiki wa Yanga wakisubiri kwa hamu kuona kama straika huyo wa Kenya atatua Jangwani au ataendelea kusalia Power Dynamos kwa msimu mwingine.

USHINDI UNAOKUJA KWA KASI YA MWANGA MVP WA UGANDA AINGIA KWENYE RADA ZA SIMBA