Yanga SC

MITEGO MITATU YA MWISHO YAITIKISA YANGA KUELEKEA UBINGWA

Vardo June 2, 2026 10:41 am

WAKATI mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara zikifikia hatua za mwisho, mabingwa watetezi Yanga wameendelea kuwa makini wakitambua kuwa bado wana kazi kubwa mbele yao katika harakati za kutetea taji lao la ligi.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kikosi hicho hakina nafasi ya kubeza mpinzani yeyote katika mechi zilizobaki, akieleza kuwa kila mchezo umebeba uzito mkubwa katika kuamua hatma ya ubingwa wa msimu huu.

Kamwe amesema tofauti na ambavyo baadhi ya watu wanavyoamini kuwa mechi dhidi ya Azam FC ndiyo itakayoamua bingwa, Yanga imejipanga kupambana katika michezo yote iliyosalia kwani kila pointi ni muhimu katika kipindi hiki cha mwisho wa msimu.

“Wapo wanaoamini hatma ya ubingwa ipo kwenye mchezo dhidi ya Azam FC, lakini sisi tunaangalia zaidi kushinda mechi zetu zote. Kila timu inapambana kutimiza malengo yake, hivyo jukumu letu ni kuhakikisha tunakusanya pointi zote zinazowezekana,” amesema Kamwe.

Ameongeza kuwa Yanga bado ipo kwenye nafasi nzuri kutokana na tofauti ya mabao iliyonayo, lakini hilo haliwapi nafasi ya kupoteza umakini kwani sare yoyote inaweza kubadilisha hesabu za ubingwa.

“Hata tukipata sare katika mchezo mmoja bado tunaweza kubaki kileleni kutokana na faida ya mabao, lakini hatutaki kufikia hatua hiyo. Lengo letu ni kushinda mechi zote zilizobaki,” amesisitiza.

Kamwe ametaja kuwa pamoja na ugumu wa mchezo dhidi ya Azam FC, bado kuna changamoto nyingine kubwa kutoka kwa TRA United na JKT Tanzania, timu ambazo zina uwezo wa kuharibu mipango ya Yanga ikiwa hazitapewa heshima inayostahili.

“Tunaweza kushinda dhidi ya Azam FC na watu wakaanza kushangilia ubingwa, lakini bado kuna TRA United ya Ramadhani Chobwedo na JKT Tanzania. Hizi ni timu ngumu ambazo zinaweza kubadilisha kila kitu kama hatutakuwa makini.

Ndiyo maana tumejielekeza kwenye kila mchezo uliobaki ili kuhakikisha hatupotezi alama na tunafikia lengo la kutwaa ubingwa,” amesema Kamwe.

MVP WA UGANDA AINGIA KWENYE RADA ZA SIMBA