ENRISO KUONGOZA NDOTO ZA PARAGUAY KOMBE LA DUNIA 2026
ASUNCION, PARAGUAY: PARAGUAY itashiriki fainali za Kombe la Dunia 2026 ikiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri baada ya kurejea kwenye mashindano hayo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2010, Afrika Kusini.
Kufuzu kwao kulizua shamrashamra kubwa nchini humo kiasi kwamba serikali ilitangaza siku ya mapumziko ya kitaifa kusherehekea mafanikio hayo yaliyokuwa yanasubiriwa kwa miaka 16.
Safari ya Paraguay kuelekea Kombe la Dunia ilijengwa juu ya misingi ambayo kwa miaka mingi imekuwa utambulisho wao mkubwa katika soka la kimataifa, uimara wa safu ya ulinzi, nidhamu ya hali ya juu na kujituma kwa kila mchezaji ndani ya uwanja.
Baada ya vipindi kadhaa vya majaribio ya kucheza soka la kumiliki mpira bila mafanikio makubwa, timu hiyo iliamua kurudi kwenye falsafa yake ya zamani iliyowahi kuipa mafanikio.
Mabadiliko makubwa yalianza mwezi Agosti mwaka 2024 wakati kocha raia wa Argentina, Gustavo Alfaro, alipopewa jukumu la kuinoa timu hiyo. Tangu siku ya kwanza alitoa ujumbe uliokuwa wazi kwa wachezaji wake kuwa mafanikio yangepatikana kwa kucheza kwa nguvu, nidhamu na kuhakikisha timu hairuhusu mabao kirahisi.
Kauli hiyo ilianza kuonekana vitendo mapema sana. Paraguay ilionekana kubadilika mara moja na kuwa timu ngumu kufungika. Wachezaji walionyesha ari kubwa ya kupambana huku wakicheza kwa mshikamano mkubwa zaidi kuliko ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.
Katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia, Alfaro alibaki mwaminifu kwa mfumo wa 4-4-2 ambao ulitoa uwiano mzuri kati ya ulinzi na ushambuliaji. Mfumo huo uliifanya Paraguay kuwa timu yenye ugumu mkubwa kuvunjwa na wapinzani wake. Mara chache sana alibadilisha mfumo huo, hasa alipokutana na mazingira magumu dhidi ya Ecuador na Bolivia.
Moja ya mafanikio makubwa ya Paraguay katika kampeni ya kufuzu ilikuwa uwezo wao wa kupata matokeo mazuri katika mazingira magumu.
Walipata sare muhimu nchini Bolivia kwenye mwinuko wa zaidi ya mita 4,000 kutoka usawa wa bahari, wakapata sare nyingine Ecuador na pia wakasimama imara dhidi ya Colombia katika mazingira ya joto kali na unyevunyevu mkubwa.
Ushindi dhidi ya Brazil na Argentina katika mechi za nyumbani uliwafanya mashabiki kuamini kuwa timu hiyo ilikuwa imerejea rasmi katika ushindani wa juu wa soka la Amerika Kusini. Matokeo hayo yaliwaondoa mashaka hata wale waliokuwa hawana imani na mradi mpya wa Alfaro.
Tiketi ya Kombe la Dunia ilipatikana baada ya sare ya bila kufungana dhidi ya Ecuador. Filimbi ya mwisho iliposikika, nchi nzima ililipuka kwa furaha huku mashabiki wakijaa mitaani kusherehekea kurejea kwa taifa lao kwenye jukwaa kubwa zaidi la soka duniani.
Ingawa Paraguay inajulikana kwa mchezo wa nguvu na ukakamavu, timu hiyo pia imeonyesha uwezo wa kucheza soka la kuvutia. Wana uwezo wa kujenga mashambulizi kutoka nyuma kwa utulivu huku wakimtegemea zaidi nyota wao Julio Enciso kubadilisha matokeo ya mchezo katika maeneo ya mwisho ya ushambuliaji.
Kocha Alfaro ndiye mtu anayesifiwa zaidi kwa mabadiliko hayo. Kocha huyo mwenye uzoefu mkubwa katika soka la Amerika Kusini amejijengea jina kwa kuzipa timu zake nidhamu ya hali ya juu ya ulinzi.
Kabla ya kujiunga na Paraguay aliwahi kuiongoza Ecuador kufuzu na kushiriki Kombe la Dunia la mwaka 2022.
Alfaro amekuwa akijulikana kama kocha anayependa falsafa za maisha na mara nyingi hutumia methali na maneno ya hekima kuelezea mipango yake ya kisoka.
Mbinu zake zimeonekana kuwagusa wachezaji wa Paraguay ambao sasa wanaonekana kucheza kwa kujiamini zaidi kuliko wakati wowote katika miaka ya karibuni.
Mchezaji anayetarajiwa kubeba matumaini makubwa ya Paraguay katika Kombe la Dunia ni Enciso. Nyota huyo anayejulikana kwa jina la utani “La Joya” yaani “Lulu”, amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa vipaji vikubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Paraguay katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.
Enciso alianza kuonyesha kipaji chake akiwa mdogo katika klabu ya Libertad kabla ya kuhamia Ulaya. Akiwa na kasi, uwezo wa kupiga chenga na kumiliki mpira vizuri, amekuwa mchezaji anayebadilisha mechi kwa muda mfupi. Licha ya kukumbwa na majeraha katika baadhi ya vipindi vya maisha yake ya soka, bado anaendelea kuwa tegemeo kubwa kwa taifa lake.
Kwa sasa Enciso anacheza soka lake nchini Ufaransa akiwa na klabu ya Strasbourg ambako ameanza kurejesha kiwango chake bora, fundi huyo aliwahi kutamba akiwa na Brighton & Hove Albion ya Ligi Kuu England.
Ndoto yake kubwa ilikuwa kucheza Kombe la Dunia na sasa ameifanikiwa baada ya kuisaidia Paraguay kufuzu.
Mbali na Enciso, macho mengi yataelekezwa kwa kiungo Damián Bobadilla. Kiungo huyo wa Sao Paulo ya Brazil amekuwa akionyesha maendeleo makubwa na sasa anatajwa kuwa mmoja wa viungo bora wa kizazi chake nchini Paraguay. Ana uwezo wa kucheza kutoka eneo moja hadi jingine la uwanja huku akisaidia kushambulia na kulinda kwa wakati mmoja.
Shujaa asiyezungumziwa sana katika kikosi hicho ni Andrés Cubas. Kiungo huyo wa kazi ngumu ndiye moyo wa timu. Kazi yake kubwa ni kuvunja mashambulizi ya wapinzani, kushinda mipira ya kugombea na kuanzisha mashambulizi mapya kwa haraka.
Licha ya kutokuwa na umbile kubwa, akili yake ya mchezo na uwezo wa kusoma mazingira humfanya kuwa muhimu sana kwa Paraguay. Mashabiki wa Paraguay nao wanatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya safari ya timu yao nchini Marekani.
Ingawa gharama za safari kuelekea Kombe la Dunia ni kubwa kwa wananchi wengi wa Paraguay, maelfu ya mashabiki wameonyesha nia ya kusafiri kwenda kuisapoti timu yao baada ya kusubiri kwa muda mrefu kurejea kwenye mashindano hayo.
Barabara za miji ambayo Paraguay itacheza mechi zake zinatarajiwa kupambwa na rangi za bendera ya taifa hilo huku nyimbo maarufu za mashabiki wa Albirroja zikisikika kila kona. Hamasa hiyo inaonyesha jinsi taifa hilo lilivyo na kiu kubwa ya kuona timu yao ikifanya vizuri katika Kombe la Dunia 2026.
Kwa kuzingatia uimara wao wa ulinzi, nidhamu ya kiuchezaji, uzoefu wa kocha Alfaro na ubora wa nyota kama Enciso, Paraguay inaingia katika Kombe la Dunia ikiwa moja ya timu zinazoweza kuleta mshangao mkubwa.
Ingawa hawapewi nafasi kubwa kama mataifa makubwa ya soka duniani, uwezo wao wa kupambana hadi dakika ya mwisho unaweza kuwafanya kuwa wapinzani hatari kwa timu yoyote watakayokutana nayo. Paraguay ipo kundi D na wenyeji Marekani, Australia na Uturuki.