PEABO BRYSON AFARIKI DUNIA AKIWA NA MIAKA 75
WASHINGATON, MAREKANI: Tasnia ya muziki wa R&B imepata pigo kufuatia kifo cha mwanamuziki mkongwe, Peabo Bryson, aliyefariki dunia juzi Jumanne, akiwa na umri wa miaka 75.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na familia yake, Bryson alifariki dunia akiwa amezungukwa na ndugu, jamaa na marafiki wa karibu. Hata hivyo, chanzo rasmi cha kifo chake hakijawekwa wazi, ingawa taarifa zinaeleza kuwa mwimbaji huyo alipata kiharusi mwishoni mwa wiki iliyopita na alikuwa akipatiwa matibabu.
Bryson ni mmoja wa wanamuziki ambao sauti zao zimetikisa muziki wa R&B kwa zaidi ya miongo mitano, akitamba kupitia nyimbo mbalimbali zilizopata mafanikio makubwa duniani. Miongoni mwa nyimbo zake maarufu ni Feel the Fire, If Ever You’re In My Arms Again, Can You Stop the Rain na Reaching for the Sky.
Alipata umaarufu zaidi kupitia ushiriki wake katika nyimbo za filamu za Disney. Mwaka 1992 alitwaa tuzo ya Grammy kwa kushirikiana na Celine Dion katika wimbo wa ‘Beauty and the Beast’, kabla ya kushinda tena mwaka uliofuata kupitia ‘A Whole New World’ aliyoimba na Regina Belle kutoka filamu ya Aladdin.
Familia ya Bryson ilieleza kuwa sauti yake ilikuwa sehemu ya kumbukumbu muhimu za maisha ya watu wengi duniani, ikiwafariji na kuwaburudisha kwa vizazi tofauti kupitia muziki wake.
“Ingawa mioyo yetu imevunjika, tunafarijika kwa upendo mkubwa alioupata na namna alivyogusa maisha ya watu wengi kupitia sauti yake na utu wake,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Hadi umauti unamkuta, Bryson alikuwa akiendelea na shughuli za muziki. Mwezi Mei mwaka huu alifanya shoo katika jimbo la Georgia, Marekani, na pia alikuwa ameandaa ziara maalumu ya Golden Touch Tour kwa ajili ya kusherehekea zaidi ya miaka 50 ya mafanikio yake katika muziki.
HISTORIA YAKE
Peabo Bryson jina lake halisi ni Robert Peapo Bryson, alizaliwa Aprili 13, 1951 katika jimbo la Kusini mwa Carolina, Marekani. Alikulia katika familia iliyopenda muziki na tangu akiwa mtoto alionyesha kipaji kikubwa cha uimbaji, akivutiwa zaidi na muziki wa soul, gospel na R&B uliokuwa ukitamba nchini humo wakati huo.
Bryson alianza safari yake ya muziki mwanzoni mwa miaka ya 1970 alipokuwa akiimba katika bendi mbalimbali za eneo la kusini mwa Marekani. Mwaka 1976 alitoa albamu yake ya kwanza iliyoitwa Peabo, hatua iliyomfungulia milango katika tasnia ya muziki wa R&B. Sauti yake ya kipekee iliyochanganya hisia za mapenzi na uwezo mkubwa wa kufikisha ujumbe ilimtofautisha na waimbaji wengi wa kipindi hicho.
Licha ya wengi kumfahamu kupitia nyimbo za Disney za Beauty and the Beast na A Whole New World, safari ya Peabo Bryson katika muziki ilianza mapema sana. Akiwa na umri wa miaka 14 tu, alianza kuimba kama mwimbaji wa nyuma (backup singer) katika bendi ya nyumbani kwao huko Greenville, Kusini mwa Carolina.
Hapo ndipo jina lake la utani la ‘Peabo’ lilipoanza kutumika baada ya viongozi wa bendi kushindwa kutamka vizuri jina lake la kuzaliwa, Peapo.
Jambo lingine ambalo wengi hawalifahamu ni kwamba kabla ya kuwa staa mkubwa, Bryson alikuwa mwandishi wa nyimbo, mtayarishaji na mpangaji wa muziki katika kampuni ya Bang Records. Alitumia miaka kadhaa akiwa nyuma ya pazia akiwaandikia na kuwaandalia kazi wasanii wengine kabla ya kupewa nafasi ya kurekodi nyimbo zake mwenyewe mwaka 1976.
Ingawa nyimbo zake za Disney ndizo zilizompa umaarufu wa kimataifa, Bryson tayari alikuwa nyota mkubwa wa R&B kabla ya hapo. Miaka ya 1970 na 1980 alijijengea jina kupitia nyimbo za mapenzi zilizomfanya atambulike kama mmoja wa waimbaji bora wa ballad nchini Marekani. Wataalamu wa muziki wanaamini mafanikio ya Disney yalikuja wakati tayari alikuwa ameshaweka msingi imara wa kazi yake.
Bryson pia alijulikana kwa uwezo wake wa kuimba duet. Tofauti na waimbaji wengi wa kizazi chake, aliweza kufanikiwa na waimbaji wanawake mbalimbali wakiwemo Roberta Flack, Regina Belle, Celine Dion na Natalie Cole. Hilo lilimfanya kuwa mmoja wa waimbaji wa kiume waliofuatiliwa zaidi.
Katika kipindi cha zaidi ya miaka 50 ya kazi yake ya muziki, Bryson alitoa zaidi ya albamu 20 na kuuza mamilioni ya nakala duniani. Mbali na mafanikio yake ya kibiashara, aliheshimika kwa uwezo wake mkubwa wa kuimba ballad za mapenzi na kufanya maonyesho ya moja kwa moja yaliyovutia mashabiki wa rika zote.
Mwaka 2019 alipata changamoto ya kiafya baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo, lakini aliendelea kurejea jukwaani na kufanya maonyesho mbalimbali. Hadi mwaka 2026, alikuwa bado akiendelea na muziki na alikuwa ameandaa ziara maalumu ya Golden Touch Tour kusherehekea zaidi ya miongo mitano ya mafanikio yake katika tasnia hiyo.