DEBORA MREMBO ANAYEBADILI TASWIRA YA NGUMI ZA KIKE TANZANIA
GLOVU mikononi, tabasamu usoni na ndoto kubwa moyoni. Hivyo ndivyo unavyoweza kumwelezea Debora George Mwenda, bondia wa kike ambaye amekuwa akivutia macho ya mashabiki wa masumbwi nchini kwa sababu mbili tofauti, kwanza uwezo wake wa kupigana ulingoni na mwonekano wake wa kuvutia nje ya ulingo.
Wakati wengi wakiamini mchezo wa ngumi ni wa wanawake wenye sura ngumu na miili ya kutisha, Debora ameifuta dhana hiyo na kuonyesha mwanamke anaweza kupigana ulingoni na wakati huohuo akabaki na haiba yake ya kike bila kuyumbishwa na mitazamo ya jamii.
Mrembo huyo mwenye umri wa miaka 27 akiwa tayari amepigana mapambano sita ya kulipwa tangu aanze safari yake mwaka 2022, anaendelea kujitengenezea jina katika uzani wa Featherweight huku akitumia ngumi kama njia ya kupambana na umaskini, kujenga maisha yake na kuhamasisha wanawake wengine kuamini katika ndoto zao.
Kwa sasa, Debora anashika nafasi ya pili nchini katika uzani wa kilo 57.15 (57.2 kg) na nafasi ya 91 duniani kulingana na rekodi za BoxRec.
Tangu alipoingia katika ngumi za kulipwa mwaka 2022, tayari amepigana mapambano sita, akishinda matatu, kutoka sare moja na kupoteza mawili.
UREMBO UNAOWACHANGANYA WENGI
Ukimwona Debora nje ya ulingo unaweza kudhani ni mwanamitindo au msanii wa filamu. Mwonekano wake wa kuvutia umekuwa ukiwashangaza wengi wanaokutana naye kwa mara ya kwanza.
Anakiri mara nyingi watu hushindwa kuamini yeye ni bondia.
“Watu wengi wakiniona kwa mara ya kwanza hawaamini kama mimi ni bondia. Wengine wanaamini ngumi ni mchezo wa wanawake wenye muonekano wa kiume zaidi, lakini ukweli, mwanamke anaweza kuwa mrembo na bado akawa bondia mzuri,” anasema Debora.
Kwa mujibu wake, dhana mwanamke anayefanya michezo ya nguvu lazima apoteze uhalisia wake wa kike ndiyo inayochangia baadhi ya wazazi kuwazuia watoto wao wa kike kushiriki michezo hiyo.
“Ninaamini inawezekana kabisa kuwa mwanamke wa kawaida, ukapenda fasheni, ukapenda kujitunza na bado ukafanya boxing kwa kiwango kikubwa. Si lazima ujibadilishe ili ukubalike kwenye mchezo huu,” anafafanua.
ALITAKA KUWA MWANAMITINDO
Kabla ya kuingia rasmi kwenye ulimwengu wa masumbwi, Debora alikuwa anapendelea zaidi uanamitindo akiamini mwonekano wake ungembeba zaidi kuliko ngumi.
“Nilikuwa na nafasi ya kufanya mambo mengi yanayohusu urembo, lakini moyo wangu ulikuwa kwenye boxing. Nilipojaribu mazoezi ya ngumi nilihisi hapo ndipo maisha yangu yalipo,” anasema.
Jina lingine maarufu ni Bondia Mrembo na hapa anaeleza ilikuwaje akajiita jina hilo “Kwanza jina hilo nilipewa na mashabiki na nikiona watu wananiita hivyo najisikia vizuri kwa sababu ni ishara wameitambua kazi yangu na safari ninayopitia,” anasema kwa tabasamu.
MWANZO WA SAFARI YAKE
Tofauti na mabondia wengi wanaoanza mchezo huo wakiwa watoto au vijana wadogo, Debora aliingia kwenye boxing akiwa na miaka 22.
Ni jambo ambalo anakiri wakati mwingine humfanya afikirie angekuwa mbali zaidi kama angeanza mapema.
“Kitu kimoja ninachojutia ni kutokuanza boxing mapema. Nahisi kama ningepata nafasi hiyo mapema ningekuwa nimekusanya uzoefu mkubwa zaidi kuliko nilionao sasa,” anasema.
Debora anaeleza alianza ubondia kama mtu anayependa kufanya mazoezi kama wanavyofanya watu wengine akiwa kwao Njombe kabla ya kuhamia Dar es Salaam.
Lakini kadri muda ulivyokwenda ndivyo alijikuta anaingia katika ngumi.
“Sikuwa na wazo kabisa la kuwa bondia ila watu niliokuwa nafanya nao mazoezi wakaniambia unaweza kuwa bondia kwa sababu ya mazoezi unayofanya na hapo ndipo karia yangu ilipoanza.”
Licha ya hilo, anaamini bado ana muda wa kutosha kujenga historia yake katika mchezo huo.
“Sijafika mwisho wa safari yangu. Bado nina malengo makubwa sana na naamini ninaweza kuyafikia kwa kufanya kazi kwa bidii,” anasema.
ALIVYOANZA HADI KUJA DAR
Anasema baada ya watu kumshawishi akawa anaendelea na mazoezi na siku moja bondia wa zamani Omari Yazidu alitembelea alipokuwa anafanya mazoezi bondia huyo na ndipo alipomwoona huko.
“Wakati anatembelea tulipokuwa tunafanya mazoezi kumbe alikuwa anajuana na baba yangu kwa sababu na yeye alikuwa bondia huko zamani ndipo akamshawishi nicheze ngumi.”
“Baada ya baba kuridhia akaniruhusu niende Dar kucheza ngumi na hiyo ndiyo ikawa na nashukuru Mungu pambano langu la kwanza nikamshinda mpinzani wangu baba akafurahi zaidi.”
FAMILIA ILIMUUNGA MKONO
Debora anasema kwa sasa familia yake inamuunga mkono lakini mwanzoni mama yake hakukubaliana na jambo hilo akiamini mchezo huo ni hatari.
“Mwanzoni mama yangu alikuwa hapendi kiukweli ila baba alinisapoti tangu siku ya kwanza. Ni mzazi na huwa anasema mchezo ni hatarishi na alishawahi kuniambia kucheza ngumi hakuna tofauti na mwanamke anayejiuza kwa sababu na wao hufanya chochote ili wapate pesa.”
Hata hivyo, anadai jamii kwa jumla bado ina safari ndefu ya kuelewa nafasi ya wanawake katika michezo.
“Familia yangu ilinisapoti vizuri tangu nilipoanza, lakini changamoto kubwa imekuwa kwa baadhi ya watu katika jamii ambao bado wanaamini boxing ni mchezo wa wanaume pekee,” anasema.
Kwa mtazamo wake, ukosefu wa uelewa huo ndiyo unaosababisha mabondia wengi wa kike kushindwa kupata sapoti wanayostahili.
“Tunahitaji jamii itambue boxing ni mchezo wa kila mtu. Mwanamke anaweza kufanya vizuri kama mwanamume akipewa nafasi na mazingira sahihi,” anasisitiza.
MAONI YA MITANDAONI HAYAMTISHI
Katika kipindi hiki ambacho mitandao ya kijamii imeshika kasi kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yake, Debora anasema amejifunza kuchuja maneno ambayo anakutana nayo mitandaoni.
Anasema kuna watu wanaompongeza na wengine wanaomkosoa, lakini ameamua kuzingatia yale yanayomjenga.
“Sina muda wa kufuatilia kila mtu anachosema kuhusu mimi. Ninaangalia yale yanayonisaidia kukua na kuyaacha yale ambayo hayana faida katika maisha yangu,” anasema.
Kwa mujibu wake, lengo kuu ni kupambana na umaskini na kujenga maisha bora kupitia kipaji chake.
“Ninafanya boxing kwa sababu ni kazi yangu. Inanisaidia kutafuta maisha na kupambana na changamoto za kiuchumi kama ilivyo kwa kazi nyingine yoyote,” anasema.
MAISHA NJE YA ULINGO
Wakati glavu zinapovuliwa na mazoezi kumalizika, Debora anasema yeye ni mwanamke wa kawaida anayependa familia, marafiki na kujifunza mambo mapya.
“Muda wangu mwingi wa mapumziko nauweka kwa familia na marafiki. Pia napenda kujifunza kuhusu biashara na namna ya kujiongezea vyanzo vya kipato,” anasema.
Anajiona kama mtu mwenye kiu ya maarifa na anayependa kuwasaidia wengine pale anapopata nafasi. “Ninaamini kila siku kuna kitu kipya cha kujifunza. Ukiacha kujifunza unakuwa umeanza kurudi nyuma,” anasema.
Lakini mbali na ngumi anasema anafanya biashara ya kuuza nguo za mazoezi na vifaa vya mazoezi.
ANA MAHUSIANO
“Nina mpenzi na mahusiano yetu yako vizuri na nashukuru anaelewa kazi yangu labda kwa sababu mwenzangu hayupo karibu, hivyo siyo mtu ambaye tunaonana mara kwa mara… hivyo hata ikitokea mechi kwake inakuwa rahisi kuelewa.”
REKODI ZAKE
Tangu aingie kwenye ngumi za kulipwa Desemba 31, 2022, Debora ameonyesha uwezo mkubwa ndani ya muda mchache tu alioingia kwenye tasnia hiyo.
Katika mapambano yake sita ya kulipwa, ameshinda matatu, kapoteza mawili na kutoka sare moja.
Pambano lake la kwanza la kulipwa ilikuwa mwaka 2022 alipomshinda Khadija Leonard kwa KO kabla ya kupata ushindi mwingine dhidi ya Neema Kalala mwaka 2024.
Mwishoni mwa mwaka 2025 alimpiga Mariam Dick kwa KO katika pambano la ubingwa wa Tanzania wa uzani wa Featherweight lililofanyika The Warehouse, Masaki jijini Dar es Salaam.
BADO SIJAKUTANA NA PAMBANO GUMU
Alipoulizwa kuhusu pambano gumu zaidi kuwahi kupigana anasema “Kwa kweli bado sijakutana na pambano gumu. Kila pambano lina changamoto zake, lakini naamini maandalizi mazuri ndiyo yananifanya niingie ulingoni nikiwa tayari,” anasema.
ANAMUIGA FRANCESCA HENNESSEY
Mwanadada huyo anasema bondia anayemfuatilia zaidi kwa sasa ni Francesca Hennessey, mmoja wa mabondia wa kike wanaokuja kwa kasi zaidi Uingereza na duniani katika uzani wa Bantamweight.
“Ninavutiwa sana na Francesca Hennessey. Namuona kama role model kwa sababu ameonyesha mwanamke anaweza kuwa na mafanikio makubwa kwenye boxing bila kupoteza utambulisho wake,” anasema.
Ndoto yake ni kufika viwango vya kimataifa na kuitangaza bendera ya Tanzania kupitia mchezo huo. “Nataka siku moja niwe miongoni mwa mabondia wanaolitangaza taifa letu duniani. Hilo ndilo lengo langu kubwa,” anasema.
UJUMBE KWA WANAWAKE
Debora anatoa ujumbe kwa wanawake “Maisha yako ni jukumu lako mwenyewe. Usisubiri mtu aje akufanyie kila kitu pambana kwa bidii, amini uwezo wako na usikubali ndoto zako zizimwe na maneno ya watu,” anasema.
Anaamini mwanamke wa kisasa anatakiwa kuwa na uwezo wa kujitegemea kiuchumi na kusimamia maisha yake mwenyewe.
“Kila mwanamke anapaswa kuwa na kipato chake na kujitengenezea njia yake ya mafanikio. Hapo ndipo uhuru wa kweli unapopatikana,” anasema.