BODI YATEGUA MTEGO LIGI KUU
BODI ya Ligi Kuu Bara (TPLB) imefanya mabadiliko kwenye muda wa michezo mitatu ya mwisho ya ligi hiyo ili kuepuka upangaji wa matokeo, lakini mashabiki kupata nafasi ya kutazama mechi za Kombe la Dunia na raundi tatu za mwisho zitachezwa muda mmoja.
Hata hivyo, mara nyingi hali hii huwapa wakati mgumu wale wanaoonyesha mpira kwenye vibanda umiza kwa kubishana ni mechi gani inatakiwa kuwekwa kati ya Simba na Yanga.
Kwa kawaida, utaratibu huo hutumika katika mechi za mwisho wa msimu pekee ili kuzuia timu kupata faida kwa kujua matokeo ya viwanja vingine.
Hata hivyo, kutokana na ushindani mkubwa wa mbio za ubingwa na vita vya kushuka daraja, kumaliza nafasi nne za juu, TPLB imeamua kuutumia pia raundi za 28, 29 na 30.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, mechi zote za raundi ya 28 zitachezwa Juni 24 kuanzia saa 10 jioni, huku raundi ya 29 ikichezwa Juni 27 kwa muda huohuo. Raundi ya mwisho ya 30 nayo itaanza saa 10 jioni Juni 30.
Hatua hiyo inalenga kupunguza uwezekano wa upangaji matokeo na kuhakikisha timu zote zinazowania ubingwa, nafasi za kushiriki michuano ya kimataifa na zile zinazopambana kubaki ligi zinashindana katika mazingira sawa.
Mbio za ubingwa bado ni kali huku mabingwa watetezi Yanga, Simba na Azam FC zikiendelea kuwa na nafasi ya kutwaa taji. Kila timu inahitaji ushindi katika mechi zilizobaki ili kuongeza matumaini ya kutimiza malengo yao.
Wakati huohuo, vita vya kujiokoa na kushuka daraja nayo imeendelea kupamba moto.
Timu za KMC, Tanzania Prisons, Mbeya City, Namungo, Mtibwa Sugar, Mashujaa, Coastal Union, Fountain Gate, Dodoma Jiji na Pamba Jiji bado zinapigania hatima yao katika ligi.
Wadau wa soka wanaamini mfumo wa mechi kuchezwa kwa wakati mmoja unapunguza uwezekano wa timu kubadili mbinu kutokana na taarifa za matokeo kutoka viwanja vingine, jambo linaloongeza haki na ushindani.
Katika raundi ya 28 kutakuwa na mechi kadhaa zenye mvuto mkubwa zikiwemo Mtibwa Sugar dhidi ya Simba, Yanga dhidi ya Azam FC na Namungo kuikaribisha KMC. Raundi ya 29 itashuhudia Azam FC ikicheza na Coastal Union, Simba kuvaana na Singida Black Stars huku Yanga ikivaana na TRA United.
Hatua hiyo ya TPLB inatarajiwa kuhakikisha msimu unamalizika kwa uwazi na ushindani wa haki, huku hatima ya ubingwa, nafasi za kimataifa na timu zitakazoshuka daraja ikiamuliwa uwanjani.
Kwa sasa zikiwa zimebaki mechi tano Yanga inaongoza kwenye msimamo ikiwa na pointi 60 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 58 huku Azam ikiwa nafasi ya tatu na pointi 52.