Azam FC

FLORENT IBENGE AIGOMEA MALI

Vardo June 3, 2026 11:10 am

DILI la kocha Mkuu wa Azam FC Florent Ibenge kwenda Mali limebuma, huku sababu kubwa ikitajwa ni bosi huyo kugoma kwenda nchini humo kwa kuwa anataka kubaki Tanzania.

Awali Mali walikuwa wameshakubaliana vitu vingi na kocha huyo raia wa DR Congo, ikiwa ni pamoja na mshahara, marupupu, ukubwa wa benchi la ufundi pamoja na malengo ya timu hiyo na vitu vyote vilishapelekwa serikalini, lakini ghafla baada ya kocha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya DR Congo kufanya kikao na mabosi wa Azam, juzi aligomea dili hilo.

Kocha huyo alipenya kwenye hatua ya mwisho ya mchujo wa makocha watano na ndiye aliyepewa nafasi kubwa ya kuchukua mikoba ya kuinoa Mali.

Katika mchujo huo, Ibenge aliwapiku makocha wengine wanne akiwemo mzawa Mohamed Magassouba, Badou Zaki wa Morocco pamoja na Wareno wawili Antonio Conceicao Oliveira na Antony Da Silva.

Wakati hayo yakiendelea, Ibenge bado ana mkataba na Azam wa mwaka mmoja wenye nafasi ya kuongeza mmoja mwingine endapo huo utamalizika.

Taarifa za ndani jana zililiambia Mwanaspoti, Ibenge amegomea dili hilo baada ya kila kitu kuwa kimeshafanyika baada ya juzi kumaliza kikao na mabosi wa Azam ambao wamekubali kumwongezea mahitaji anayoyataka.

“Ibenge alikuwa na kikao kizito na viongozi wa Azam baada ya taarifa ya kukubaliwa maombi yake na Mali, nadhani hicho ndicho kimebadili upepo wake wa kutaka kuondoka mwishoni mwa msimu huu.

“Sasa anasalia Azam kwani mabosi walitaka kumwongeza mkataba wa miaka miwili zaidi, ambao utampa uhakika wa kuwa naye kwa muda mrefu zaidi, kwani ni kocha bora.”

Ndani ya Ligi Kuu Bara, timu ambazo zimeanza na kocha mmoja msimu huu na kwenda naye mwishoni mwa msimu ni Azam FC, JKT Tanzania, Pamba Jiji pekee, lakini si hivyo Ibenge ameweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kuifikisha Azam hatua ya makundi Kombe la Shirikisho kwa sasa ikiwa nafasi ya tatu kwenye ligi.

SINGIDA BLACK STARS YAMFUNGIA KAZI MSAUZI BODI YATEGUA MTEGO LIGI KUU