MWAKINYO AFUNGUKA SABABU ZA KUPOTEZA PAMBANO LA IBO
Bondia nyota wa Tanzania, Hassan Mwakinyo, amesema udhaifu wa mwili na kushindwa kucheza katika kiwango chake cha kawaida ndiyo sababu kubwa iliyochangia kupoteza pambano lake la kuwania mkanda wa IBO dhidi ya Michel Soro wa Ivory Coast.
Mwakinyo alipoteza pambano hilo kwa Technical Knockout (TKO) katika raundi ya tisa ya pambano la raundi 12 la uzani wa middleweight lililopigwa kwenye ukumbi wa Parc Des Expositions jijini Abidjan, Ivory Coast.
Akizungumza baada ya pambano hilo, Mwakinyo aliwaomba radhi mashabiki wake wote waliohuzunika kutokana na matokeo hayo, akisisitiza kuwa hataki kutafuta sababu za kujitetea bali kueleza hali halisi aliyokuwa nayo kabla na wakati wa pambano.
“Napenda nitoe pole za maumivu kwa wote mlio umizwa au kutokuelewa kilichotokea jana. Siyatetei matokeo ya kupoteza kwangu na siumii sababu, ndiyo game. Kinachoniumiza zaidi ni mimi kuwa weak kiasi cha kushindwa kujitetea. Hata namna ya upiganaji wangu haikuwa ile mliyoizoea,” alisema Mwakinyo.
Alieleza kuwa licha ya kufanya maandalizi makubwa na mazoezi mazito ya nguvu kuelekea pambano hilo, aliingia ulingoni akiwa dhaifu na mwepesi zaidi ya kiwango alichokizoea, jambo lililoathiri uwezo wake wa kupambana.
“Ilikuwa game tough ambayo niliweka bidii zangu kwenye mazoezi ya nguvu sana na ndiyo game ambayo nilicheza nikiwa niko weak na mwepesi sana. Yote kwa yote ni matokeo tu na hakuna budi kuyapokea,” aliongeza.
Kupoteza kwa Mwakinyo dhidi ya Soro kunakuwa ni mara ya tatu kwake kushindwa kwa knockout katika maisha yake ya ngumi za kulipwa, huku ndoto yake ya kutwaa mkanda wa IBO zikigonga mwamba mbele ya bondia huyo mwenye uzoefu mkubwa kutoka Ivory Coast.