Simba SC

SIMBA YAMLIPA SH.120M MSIMU, ASAINI MKATABA WA MIAKA MIWILI

Vardo June 11, 2026 1:20 pm

KIUNGO Bakari Msimu ameamua kujiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kushawishiwa na ofa nono inayodaiwa kufikia Sh milioni 120 pamoja na mshahara mkubwa, hatua inayofungua ukurasa mpya katika maisha yake ya soka.

 

Msimu amefikia uamuzi huo baada ya kukataa kuongeza mkataba wake na Coastal Union FC, licha ya juhudi za viongozi wa klabu hiyo kumshawishi kubaki kwa muda mrefu zaidi.

Taarifa kutoka ndani ya Coastal Union zinaeleza kuwa uongozi wa timu hiyo ulikuwa katika hatua za mwisho za kumuandalia mkataba mpya kwa lengo la kumbakiza kikosini na baadaye kunufaika kupitia mauzo yake. Hata hivyo, nyota huyo aliamua kutafuta changamoto mpya nje ya klabu hiyo.

Inaelezwa kuwa sababu kubwa iliyomvutia Msimu kuhamia Simba ni hamu yake ya kucheza katika kiwango cha juu zaidi, sambamba na kupata nafasi ya kushiriki mashindano makubwa ya kimataifa ambayo Wekundu wa Msimbazi hushiriki mara kwa mara.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, kiungo huyo amesaini mkataba wa miaka miwili ambapo katika mwaka wa kwanza atakuwa akilipwa mshahara wa Sh milioni sita kwa mwezi. Mwaka wa pili mshahara wake utaongezeka na kufikia Sh milioni saba kwa mwezi.

Mbali na mshahara huo, Msimu pia atanufaika na ada ya usajili ya Sh milioni 120, jambo linaloonyesha dhamira ya Simba kuwekeza kwa nguvu katika huduma zake kuelekea maandalizi ya msimu mpya wa mashindano.

Usajili wa Msimu ni sehemu ya mkakati wa Simba wa kuimarisha kikosi chake katika maeneo mbalimbali muhimu. Benchi la ufundi linaendelea kutathmini wachezaji watakaosaidia kuongeza ushindani ndani ya timu hiyo huku ikijiandaa kwa changamoto za msimu ujao.

TAHADHARI KALI KWA MASHABIKI WANAOSAFIRI KOMBE LA DUNIA SIMBA YAVUNJA UKIMYA KUHUSU FEI TOTO, YATOA KAULI NZITO