Simba SC

SIMBA YAVUNJA UKIMYA KUHUSU FEI TOTO, YATOA KAULI NZITO

Vardo June 11, 2026 1:30 pm

MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema klabu hiyo ingependa kuwa na kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, lakini amesisitiza kuwa si jambo rahisi kutokana na mchezaji huyo kuwa chini ya mkataba na klabu yake ya sasa.

 

Kauli hiyo ya Ahmed inakuja wakati ambapo kumekuwa na taarifa zinazoenea zikidai kuwa Fei Toto amegomea kuongeza mkataba mpya Azam FC, hali iliyozua mijadala kuhusu hatma yake na kuhusishwa na klabu mbalimbali ikiwemo Simba.

Ripoti hizo zimeeleza kuwa baadhi ya timu zimeanza kufanya tathmini ya uwezekano wa kumsajili kiungo huyo ambaye amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi katika Ligi Kuu Tanzania Bara kwa misimu ya karibuni.

Akizungumzia suala hilo, Ahmed amesema ni kawaida kwa klabu kubwa kuvutiwa na wachezaji wenye ubora wa hali ya juu, huku akimtaja Fei Toto kuwa miongoni mwa viungo bora nchini kwa sasa.

Amesema uwezo wa mchezaji huyo ndani ya uwanja ni wa kipekee na kwamba ana sifa zinazoweza kuifanya timu yoyote kuwa imara zaidi katika eneo la kiungo.

“Hakuna timu ambayo haitamtamani Feisal. Ni mchezaji mkubwa, mwenye ubora mkubwa na anayetoa kile ambacho mashabiki na benchi la ufundi wanakitarajia kutoka kwa mchezaji wa kiwango chake,” amesema Ahmed.

Hata hivyo, Ahmed amesisitiza kuwa kwa sasa Simba haiwezi kufanya lolote kuhusu mchezaji huyo kwa kuwa bado ni mali ya Azam FC.

“Simba SC tunatamani kuwa na mchezaji kama Feisal kwa sababu ni top player, lakini hatuwezi kwa sababu si mchezaji wetu, ni mali ya Azam FC,” ameongeza.

SIMBA YAMLIPA SH.120M MSIMU, ASAINI MKATABA WA MIAKA MIWILI