SIMBA KAZI ANAYO BARKER AWASILISHA ORODHA YA WACHEZAJI ANAOWATAKA
BODI ya Wakurugenzi ya Simba chini ya Mwenyekiti wake, Crescentius Magori, inakabiliwa na jukumu kubwa la kuhakikisha mahitaji ya benchi la ufundi yanatekelezwa baada ya Kocha Mkuu, Steve Barker, kuweka wazi kuwa tayari ameanza mchakato wa kuimarisha kikosi kwa ajili ya msimu ujao.
Barker amesema benchi lake la ufundi limeanza rasmi kazi ya kutafuta wachezaji wapya watakaoongeza ushindani na ubora ndani ya kikosi, huku baadhi ya majina ya nyota wanaohitajika tayari yakiwasilishwa kwa uongozi kwa ajili ya hatua za usajili.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini ameeleza kuwa licha ya kuridhishwa na kiwango kinachoonyeshwa na wachezaji waliopo, bado kuna umuhimu wa kufanya maboresho ili kuiweka Simba katika nafasi nzuri ya kuendelea kushindana kwa mafanikio kwenye mashindano ya ndani na yale ya kimataifa.
Amesisitiza kuwa tathmini ya maeneo yanayohitaji kuongezewa nguvu bado inaendelea, akibainisha kuwa timu kubwa kama Simba haiwezi kutegemea mafanikio ya sasa pekee bila kuendelea kujiboresha kila msimu.
“Tumeshanza kufanya kazi ya usajili, lakini siwezi kuzungumzia majina ya wachezaji tunaowafuatilia kwa sasa. Huo ni mchakato unaoendelea,” amesema Barker.
Mbali na mipango ya dirisha lijalo la usajili, Barker ameeleza kufurahishwa na mchango wa wachezaji waliosajiliwa katika dirisha dogo la Januari, akisema wameongeza ushindani ndani ya kikosi na kuwa sehemu muhimu ya mafanikio ambayo timu imepata msimu huu.
Akizungumzia ushindani wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kocha huyo amesema kiwango cha ushindani kimeongezeka kwa kiasi kikubwa, jambo linaloifanya Simba kuongeza umakini na bidii katika kila mchezo ili kuendelea kubaki kwenye mbio za mafanikio.
Kuhusu mashindano ya kimataifa, Barker amesema Simba bado ina ndoto kubwa ya kufika mbali zaidi na kupambana katika hatua za juu.
Amebainisha kuwa kutwaa mataji kunahitaji maandalizi ya kina, ikiwemo kufanya usajili wa wachezaji wenye uwezo mkubwa, nidhamu na kiu ya mafanikio ili kuisaidia klabu kufikia malengo yake makubwa katika misimu ijayo.