Azam Wavunja Ukimya, Sababu Ya Kususia Medali Fainali
MMILIKI wa Azam FC, Jamal Bakhresa, ameibua mjadala mkubwa baada ya kuikosoa timu ya waamuzi kufuatia kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Simba SC katika fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB.
Mchezo huo wa fainali ya CRDB Federation Cup ulipigwa katika dimba la Gombani, Pemba, na kushuhudia Simba wakitwaa ushindi mwembamba baada ya beki wa Azam, Yahya Zaid, kujifunga bao lililoamua matokeo ya mchezo.
Azam FC walizidi kupata wakati mgumu zaidi baada ya kiungo wao Feisal Salum kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja, kufuatia tukio lililohusisha kumpiga kiwiko mshambuliaji wa Simba, Libasse Gueye, hali iliyoibua malalamiko makubwa kutoka benchi la ufundi la Azam.
Baada ya tukio hilo, wachezaji pamoja na benchi la ufundi la Azam FC walionekana kutoridhishwa na maamuzi ya mwamuzi, hatua iliyowapelekea kususia kwenda kuchukua zawadi za washindi wa pili, ikiwemo medali zao.
Akizungumza kuhusu hali hiyo, Bakhresa amesema hakuridhishwa na baadhi ya maamuzi ya waamuzi, akisisitiza kuwa ataendelea kulizungumzia suala hilo ili kusaidia kuboresha kiwango cha uamuzi katika msimu ujao.
“Hatukwenda kuchukuwa medali wala zawadi yoyote pale mbele. Timu yangu ya Azam FC haijaenda kupokea zawadi bali aliyeenda ni Mtendaji Mkuu,” amesema Jamal.
Amesitiza kuwa sheria za mchezo zinapaswa kutafsiriwa kwa usawa kwa timu zote bila upendeleo, akionya kuwa endapo maamuzi yenye utata yataendelea, yanaweza kudhoofisha maendeleo ya soka nchini na kupunguza imani ya wadau katika mchezo huo.
Kwa upande mwingine, ameikosoa pia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF, akidai halijawekeza vya kutosha katika kuwajengea uwezo waamuzi, huku akiongeza kuwa Azam FC ipo tayari hata kushiriki mashindano ya Zanzibar iwapo itaadhibiwa kutokana na ukosoaji wake.