Kutwaa Ubingwa CRDB, Mpanzu Atuma Onyo Kwa Wapinzani
KIUNGO wa Simba, Elia Mpanzu, amesema kikosi chao kilistahili kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB kutokana na kiwango bora na juhudi walizoonyesha tangu hatua za awali za mashindano hadi mchezo wa fainali.
Mpanzu amesema tangu mashindano yalipoanza, wachezaji waliweka lengo la kuhakikisha wanamaliza msimu kwa kutwaa taji hilo, jambo ambalo wamefanikiwa kulitimiza baada ya kupambana kwa kujituma katika kila hatua ya safari yao.
Ameeleza kuwa safari ya kuelekea ubingwa haikuwa nyepesi kutokana na ushindani mkubwa waliokutana nao kutoka kwa wapinzani mbalimbali, lakini mshikamano, nidhamu na ari ya ushindi vilikuwa nguzo muhimu zilizowasaidia kufika fainali na hatimaye kutwaa kombe hilo.
“Tulistahili kupata kombe hili. Tulipambana kuanzia hatua ya kwanza hadi fainali. Tulikutana na timu ngumu hadi kufikia hatua ya fainali na hatimaye kutwaa taji hili,” amesema Mpanzu.
Kiungo huyo amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mkubwa kati ya benchi la ufundi na wachezaji, ambapo kila mmoja alitimiza wajibu wake kwa lengo la kuhakikisha Simba inafikia malengo waliyojiwekea mwanzoni mwa msimu.
Ameongeza kuwa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB umewapa hamasa na kujiamini zaidi kuelekea maandalizi ya msimu wa 2026/27, wakilenga kuendelea kufanya vizuri katika mashindano yote watakayoshiriki.
Mpanzu amehitimisha kwa kuwashukuru mashabiki wa Simba kwa sapoti yao isiyoyumba msimu mzima, huku akiwaahidi kuwa kikosi hicho kitaendelea kupambana kwa nguvu zote ili kuwania mataji mengi zaidi, yakiwemo ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano mengine katika msimu ujao.