Wanaomvizia Nzengeli WabainikaBado Yupo Sana Yanga
KIUNGO wa Yanga SC, Max Nzengeli, ameweka wazi msimamo wake kuhusu hatma yake ndani ya kikosi hicho, akisisitiza kuwa bado yupo tayari kuendelea kupambana kwa ajili ya mafanikio zaidi katika msimu ujao wa mashindano.
Nyota huyo amesema anaendelea kuwa sehemu muhimu ya mipango ya klabu hiyo, huku akiahidi yeye na wenzake kuongeza bidii kuhakikisha Yanga SC inaendelea kufanya vizuri katika mashindano yote itakayoshiriki.
Nzengeli amebainisha kuwa mafanikio yaliyopatikana katika miaka ya hivi karibuni yametokana na mshikamano mkubwa uliopo ndani ya timu, akisema hilo ndilo siri kubwa ya mafanikio yao.
“Mafanikio tuliyoyapata kwa miaka mitano ni kutokana na umoja na ushirikiano. Sisi wachezaji tutatekeleza wajibu wetu uwanjani kuhakikisha tunawapa mashabiki furaha msimu ujao,” amesema Nzengeli.
Ameongeza kuwa ana imani kubwa ya kuendelea kubaki ndani ya kikosi hicho, akieleza kuwa uongozi wa klabu umekuwa ukimpa imani na sapoti ya kutosha kuelekea msimu mpya.
Pia ametoa wito kwa mashabiki wa Young Africans SC kuendelea kushikamana na timu hiyo, akisisitiza kuwa mchango wao nje ya uwanja ni muhimu sawa na juhudi za wachezaji uwanjani.
Kwa mujibu wa kiungo huyo, ushirikiano kati ya wachezaji na mashabiki ndio msingi mkuu unaoweza kuiwezesha Yanga kuendelea kubaki kileleni na kuongeza mafanikio zaidi katika mashindano ya ndani na yale ya kimataifa.