Aziz Ki Aibua Maswali Mapya Kuhusu Usajili Wake
BAADA ya kuhusishwa na tetesi za kurejea Yanga kwa mara nyingine, kiungo wa Al-Ittihad ya Libya, Stephane Aziz Ki, amesema kwa sasa hawezi kuzungumzia mustakabali wake kwani yupo nchini kwa ajili ya mapumziko baada ya kumalizika kwa msimu wa ligi.
Aziz Ki amekuwa akihusishwa na kurejea ndani ya kikosi cha Yanga, huku taarifa zikidai kuwa makubaliano kati yake na klabu hiyo yamefikiwa, kinachosubiriwa kikiwa ni hatua za mwisho zinazohusisha klabu yake ya Al-Ittihad ya Libya.
Akizungumza akiwa nchini Tanzania, nyota huyo amesema kipindi hiki ni cha mapumziko na tetesi za usajili ni jambo la kawaida katika dirisha la usajili.
“Nipo Tanzania kwa ajili ya mapumziko yangu ya likizo baada ya ligi kumalizika. Kuhusu tetesi za usajili, huwezi kuzikwepa kwa sababu hiki ndiyo kipindi chake,” amesema Aziz Ki.
Kiungo huyo kwa sasa yupo nchini na jana alishiriki mchezo wa hisani wa Wape Tabasamu uliofanyika mkoani Morogoro, ulioratibiwa na Dickson Job kwa kushirikiana na Kibwana Shomari, ambapo alijumuika na mastaa mbalimbali wa soka katika kusaidia shughuli za kijamii