SH670 Bilioni Kumfungia Wembanyama Spurs
SAN ANTONIO, MAREKANI: KLABU ya San Antonio Spurs imeonyesha wazi imejipanga kujenga timu yake kwa muda mrefu baada ya kumfunga nyota wake Victor Wembanyama mkataba mpya wa miaka mitano wenye thamani ya dola milioni 252 (zaidi ya Sh670 bilioni).
Licha ya kuwa na nafasi ya kusaini mkataba wa kiwango cha juu zaidi (supermax) wenye asilimia 30 ya kikomo cha mishahara, nyota huyo wa Kifaransa alikubali kusaini mkataba wa kiwango cha asilimia 25, hatua iliyosaidia Spurs kuendelea kuwa na nafasi ya kuboresha kikosi chake.
Ripoti zinaeleza Wembanyama hata alikuwa akifikiria kusaini kwa kiwango cha chini kuliko kiwango cha juu alichostahili kupata, jambo linaloonyesha dhamira yake ya kuendelea kuijenga Spurs badala ya kuangalia fedha pekee.
Awali, wachambuzi wa NBA walikuwa wameeleza hakutakuwa na mazungumzo magumu kuhusu mkataba huo kutokana na umuhimu wa mchezaji huyo ndani ya klabu. Pia ilielezwa mkataba huo unaweza kuongezeka hadi dola milioni 303.3 endapo atatimiza vigezo mbalimbali, ikiwemo kuchaguliwa kwenye kikosi bora cha NBA, kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Kujihami (Defensive Player of the Year) au MVP.
Wembanyama angeingia katika hadhi ya mchezaji mwenye masharti maalumu ya uhamisho (restricted free agent) baada ya msimu wa 2026-27, lakini Spurs haikutaka kufikia hatua hiyo na iliamua kumaliza suala hilo mapema.
Tangu ilipomchagua kwa namba moja katika NBA Draft ya mwaka 2023, Wembanyama ameendelea kuthibitisha kuwa ndiye nguzo mpya ya Spurs. Katika msimu wake wa kwanza alitwaa tuzo ya Rookie of the Year, akachaguliwa kwenye Kikosi Bora cha Walinzi na kuongoza ligi kwa wastani wa vizuiaji 3.6 kwa kila mchezo.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 22 alimaliza msimu akiwa na wastani wa pointi 25.0, reboundi 11.5, pasi za mwisho 3.1, vizuiaji 3.1 na kuiba mpira mara 1.0 kwa kila mchezo. Pia alifunga kwa asilimia 51.2 ya mashuti ya kawaida na asilimia 34.9 ya mashuti ya pointi tatu.