Michezo Bongo

Lwasa Aivulia Kofia Ligi Kuu

Vardo July 12, 2026 9:15 am

ALIYEKUWA kiungo mshambuliaji wa Pamba Jiji, Mganda Peter Lwasa amesema Ligi Kuu ya Tanzania ndiyo iliyomfanya kuonekana zaidi na kupata dili la kujiunga na G.D. Interclube inayoshiriki Ligi Kuu ya Angola ya Girabola na wala sio vinginevyo.

Akizungumza na Soka La Bongo, Lwasa alisema kucheza misimu miwili katika Ligi Kuu Bara kumempa heshima kubwa zaidi kwake ya kuonekana nje ya mipaka ya Tanzania, jambo ambalo ataendelea kulikumbuka maishani mwake kutokana na fursa aliyoipata.

“Nimefurahia kufungua ukurasa mpya katika maisha yangu nje ya Tanzania lakini nashukuru pia kwa sapoti kubwa niliyopata kipindi chote nilichocheza Ligi Kuu Bara, kwani ilikuwa ni chachu ya kuonekana na kupata fursa nyingine,” alisema Lwasa.

Aidha, nyota huyo alisema licha ya uongozi wa Pamba Jiji kumuwekea ofa mpya ya kuongeza mkataba mwingine baada ya huu wa sasa kumalizika msimu wa 2025-2026, ila aliona ni vyema kutafuta changamoto sehemu nyingine, licha ya thamani aliyopewa.

“Ni kweli uongozi wa Pamba ulitaka niendelee nao msimu wa 2026-2027, ila niliwaomba nikatafute changamoto sehemu mpya nje ya Tanzania, nashukuru walinielewa na kunitakia kila la heri, nawashukuru sana kwa ukarimu walionionyesha,” alisema.

Kwa mara ya kwanza nyota huyo alitua nchini na kujiunga na Kagera Sugar Agosti 15, 2024 akitokea KCCA FC ya kwao Uganda, ambapo kwa msimu wa 2024-2025, akiwa na timu hiyo alionyesha kiwango kizuri na kuifungia mabao manane ya Ligi Kuu Bara.

Kwa msimu wa 2025-2026, aliifungia Pamba Jiji mabao matatu ya Ligi Kuu Bara, huku akizichezea pia URA FC na KCCA FC zote za kwao Uganda, Sofapaka FC, FC Kariobangi Sharks na Gor Mahia FC za Kenya, kisha kucheza Lubumbashi Sports ya DR Congo.

Geita Yamtaka Winga Yanga Mnigeria Mambo Magumu Azam