Kocha Yanga Aaga Kwa Waraka Mrefu, Akisubiriwa Uarabuni
Kocha Msaidizi wa Yanga, Matthew Silva ameaga rasmi ndani ya klabu hiyo jambo linaloonekana kuchangiwa na sababu mbili za msingi.
Matthew ameandika waraka mrefu wa kuaga akisema ndoto zake zimetimia.
“Ninaondoka Yanga kwa namna ambavyo siku zote nilikuwa nikiota. Lengo langu lilikuwa kuondoka nikiwa mtu mwenye utu, mkarimu, mwenye moyo mwema, mwenye nia njema, mchapakazi, aliyejitolea, mwenye shauku, makini, mwenye uwezo na mtaalamu wa kweli. Na kwa furaha kubwa, lengo hilo limetimia.
“Ni kwa misingi hiyo pekee tuliweza kuwa na ndoto na dhamira ya kumaliza msimu tukiwa mabingwa wa kihistoria kwa mara ya tano mfululizo.
Matthew ameishukuru klabu hiyo kwa namna imekuwa ikisapoti benchi la ufundi.
“Kwa viongozi wote wa klabu na timu nzima inayofanya kazi kila siku bila kuchoka kuhakikisha klabu inaendelea kupiga hatua kwa kasi kubwa na kuweka mazingira bora ya kupigania malengo makubwa, asante sana.
“Kwa benchi lote la ufundi na makocha wote ambao mmejitolea na kupambana kila siku ili kuhakikisha historia inaandikwa kupitia kujituma kusikochoka na kazi kubwa inayofanyika nyuma ya pazia kwa heshima na weledi, nawashukuru sana.
“Na mwisho kabisa, kwa Wananchi wote popote mlipo. Msaada wenu hauna kikomo, Haujaenea tu kila kona ya Tanzania, wala Afrika Mashariki pekee kama klabu kubwa na bora zaidi, wala Afrika tu, bali umefika duniani kote,” amesema Matthew.