Geita Yamtaka Winga Yanga
MABOSI wa Geita Gold wamefungua mazungumzo na mabingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026, Klabu ya Yanga kwa lengo la kumrejesha aliyekuwa winga nyota wa kikosi hicho, Edmund John kutokana na kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara.
“Edmund ni miongoni mwa wachezaji tunaoamini wanaweza kutusaidia kwa msimu ujao kutokana na uzoefu wake na isitoshe pia Geita ni nyumbani, makubaliano yaliyopo ni ya mkopo kwa sababu hatutaweza kuvunja mkataba wake,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisema uzoefu wa mchezaji huyo ni chachu ya kuongeza ushindani msimu ujao, ambapo kwa sasa mabosi wa timu hiyo wamejipanga kuongeza wachezaji wengi watakaoleta morali ya kukipambania kikosi hicho katika mashindano mbalimbali.
Edmund aliwahi kuitumikia Geita Gold msimu wa 2023-2024, huku akikumbukwa zaidi baada ya kuifungia timu hiyo bao moja la Ligi Kuu, katika ushindi wa kikosi hicho wa 1-0, dhidi ya maafande wa JKT Tanzania, mechi iliyopigwa, Novemba 22, 2023.
Kiwango bora alichokionyesha nyota huyo, kikawavutia mabosi wa Singida Black Stars iliyomsajili kwa msimu wa 2024-2025 na Agosti 14, 2025, alijiunga rasmi na Yanga, ingawa amekosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza kutokana na ushindani.