news

Simba Yamnasa Badjo, Barker Apata Ukuta Mpya

Vardo July 12, 2026 1:43 pm

KATIKA kuendelea kujiimarisha kuelekea msimu wa 2026/27, uongozi wa Simba umekamilisha usajili wa beki wa kati raia wa Ivory Coast, Serge Badjo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha safu ya ulinzi kabla ya kuanza kwa msimu mpya.

Taarifa zinaeleza kuwa Badjo amejiunga na Wekundu wa Msimbazi baada ya mazungumzo ya muda mrefu yaliyohusisha benchi la ufundi likiongozwa na Kocha Mkuu Steve Barker, ambaye alifuatilia uwezo wa beki huyo na kuridhishwa na kiwango chake kabla ya kutoa idhini ya usajili kukamilishwa.

Kwa mujibu wa chanzo cha ndani, usajili wa Badjo ni sehemu ya mapendekezo ya benchi la ufundi yanayolenga kuongeza ushindani katika nafasi ya beki wa kati, ili kumpa Barker chaguo pana la wachezaji kulingana na mahitaji ya kila mchezo na mashindano.

Badjo, ambaye aliwahi kuitumikia MC Alger, anafahamika kwa uimara wake katika ukabaji, utulivu akiwa na mpira pamoja na uwezo mkubwa wa kusoma mchezo. Simba inaamini sifa hizo zitaiwezesha kuimarisha zaidi safu yake ya ulinzi katika mashindano ya ndani na yale ya kimataifa.

Aidha, ujio wa beki huyo umechochewa na pengo lililoachwa na Rushine De Reuck, anayetarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu kutokana na jeraha kubwa alilopata.

Kwa kukamilisha usajili wa Badjo, Simba inaendelea kuonyesha dhamira yake ya kujenga kikosi chenye ushindani mkubwa kitakachowania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho pamoja na kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa msimu wa 2026/27.

SH670 Bilioni Kumfungia Wembanyama Spurs Aziz Ki Aibua Maswali Mapya Kuhusu Usajili Wake