Ofa Zimejaa kwa Mwamnyeto, Uamuzi Waja Baada Ya Julai 15
BEKI wa Bakari Mwamnyeto anatarajiwa kuweka wazi hatma yake ya kubaki au kuondoka Yanga mara baada ya kumalizika kwa mechi ya hisani ya Mwamnyeto Foundation, itakayochezwa Jumatano, Julai 15, 2026.
Beki huyo amemaliza mkataba wake wa miaka sita ndani ya Yanga tangu alipojiunga na klabu hiyo mwaka 2020 akitokea Coastal Union, huku hadi sasa akiwa hajafikia makubaliano ya kusaini mkataba mpya.
Meneja wake, Carlos Sylivester maarufu kama Mastermind, amesema kwa sasa wameamua kuweka pembeni masuala ya usajili na kuelekeza nguvu zote katika maandalizi ya mechi hiyo ya hisani, kabla ya kufanya uamuzi kuhusu hatua inayofuata ya mchezaji huyo.
“Ni kweli Mwamnyeto amemaliza mkataba na Yanga na bado hajaongeza. Kwa sasa tunasubiri amalize jambo lake la mechi ya hisani, kisha tutakaa na kupitia ofa zote zilizopo mezani,” amesema Mastermind.
Amefafanua kuwa baada ya mchezo huo watayachambua kwa kina mapendekezo kutoka klabu mbalimbali kabla ya kufikia uamuzi wa mwisho kuhusu timu ambayo Mwamnyeto ataitumikia katika msimu wa 2026/27.
Pamoja na kuwepo kwa ofa hizo, Mastermind ameweka wazi kuwa chaguo lao la kwanza ni kuona Mwamnyeto akiendelea kuvalia jezi ya Yanga, iwapo mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya yatazaa matunda na pande zote kufikia mwafaka.