Simba SC

Siri Yafichuka! Simba Yatoa Sababu ya Kuachana na Kambi ya Nje

Vardo July 12, 2026 11:44 pm

SIMBA imeeleza sababu ya kutokwenda nje ya Tanzania kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya msimu wa 2026/27, ikibainisha kuwa muda mfupi uliobaki kabla ya kuanza kwa mashindano ndiyo umechangia uamuzi huo.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema badala ya kuweka kambi nje ya nchi kama ilivyokuwa katika misimu iliyopita, Simba itashiriki Mashindano ya CECAFA yatakayofanyika nchini Rwanda kama sehemu ya maandalizi ya msimu mpya.

Ahmed amesema ni zaidi ya miaka saba au nane imepita tangu Simba iliposhiriki mashindano hayo, hivyo safari hii yatachukuliwa kama sehemu ya programu ya pre-season kwa lengo la kukiandaa kikosi kuelekea msimu wa 2026/27.

“Tunaenda kushiriki mashindano ya CECAFA yatakayofanyika Rwanda. Zaidi ya miaka saba au nane hatukushiriki mashindano hayo, lakini sasa tunayatumia kama pre-season,” amesema Ahmed.

Amefafanua kuwa ratiba ya maandalizi ni fupi, jambo lililosababisha benchi la ufundi linaloongozwa na Steve Barker kwa kushirikiana na uongozi wa klabu kuamua kuyatumia mashindano hayo kuwapa wachezaji mechi za ushindani na kuongeza utimamu wa mwili kabla ya kuanza kwa ligi.

“Hatuna muda mrefu kabla ya kurejea kwenye ligi, hivyo benchi la ufundi na uongozi wameona ni bora kutumia mashindano hayo kama sehemu ya maandalizi ya msimu ujao,” amesema.

Uamuzi huo unatarajiwa kuisaidia Simba kujenga kikosi chake mapema kupitia mechi za ushindani, huku ikijiandaa kwa kampeni za mashindano ya ndani na kimataifa katika msimu wa 2026/27.

Yanga Yapambana na FAR Rabat, Al Ahly Tripoli Kumuwania Lilepo Ofa Zimejaa kwa Mwamnyeto, Uamuzi Waja Baada Ya Julai 15