Yanga Yapambana na FAR Rabat, Al Ahly Tripoli Kumuwania Lilepo
UONGOZI wa Yanga unatajwa kuwa katika mazungumzo ya mwisho ya kumsajili winga wa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Makabi Lilepo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha kikosi kuelekea msimu wa 2026/27.
Taarifa zinaeleza kuwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara wanaendelea kusukuma kwa nguvu kukamilisha dili hilo mapema, huku kocha mkuu mpya, Manqoba Mngqithi, akidaiwa kuwa miongoni mwa wanaosisitiza usajili wa nyota huyo kutokana na uwezo wake wa kuongeza makali na ushindani katika safu ya ushambuliaji.
Lilepo, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) mwenye umri wa miaka 28, amezua gumzo baada ya kutosafiri na kikosi cha Kaizer Chiefs kilichoelekea Hispania kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya, jambo lililozidisha tetesi za kuondoka kwake ndani ya klabu hiyo.
Mbali na Yanga, taarifa zinaeleza kuwa klabu za FAR Rabat ya Morocco na Al Ahly Tripoli ya Libya pia zimeonyesha nia ya kuwania saini ya winga huyo, hali inayoongeza ushindani katika harakati za kumpata.
Hata hivyo, Yanga inaelezwa kuendelea na mazungumzo kwa kasi ikiwa na lengo la kukamilisha usajili huo kabla ya kuanza rasmi kwa maandalizi ya msimu mpya, ili Mngqithi aanze kazi akiwa na kikosi alichokikusudia.