Burudani

Esma Platnumz Awajibu Waliotaja Watoto Wa Diamond

Vardo July 13, 2026 3:19 pm

BAADA ya kauli yake ya hivi karibuni kutafsiriwa tofauti na baadhi ya mashabiki, Esma Platnumz ameweka wazi alichomaanisha aliposema kaka yake, Diamond Platnumz ana watoto watatu, akisisitiza hakusema ni mtoto gani ni wake na yupi si wake.

Kauli hiyo ya Esma ilianza kujadiliwa baada ya mahojiano yake na Wasafi TV na alipoulizwa Diamond ana watoto wangapi amesema ana watoto watatu. Jibu hilo lilizua maswali kwa baadhi ya mashabiki waliotaka kufahamu kama mtoto wa mwanamitindo Hamisa Mobetto, Dylan alihesabiwa kwenye idadi hiyo au la.

Baadhi ya mashabiki walitafsiri watoto watatu aliowataja Esma ni wale wanaofahamika zaidi hadharani, huku wakijiuliza sababu ya mtoto wa Hamisa kutotajwa kwenye orodha hiyo. Kutokana na tafsiri hizo, Mwanaspoti lilimtafuta Esma ili kufahamu maana halisi ya kauli yake.

Esma ameliambia Mwanaspoti  hakumaanisha kumtaja mtoto yeyote kuwa ni wa Diamond au si wake, bali alitoa jibu kutokana na swali aliloulizwa na watu wameanza kuongeza tafsiri zao.

“Mimi nilisema Diamond ana watoto watatu, ila sikusema huyu yupo ni wake na huyu hayupo ni wake. Watu waache uchonganishi na kutafsiri tofauti kile mtu anachozungumza,” amesema Esma Platnumz.

Esma alisisitiza maneno yake yameeleweka tofauti na alivyokusudia, huku akitaka watu kuangalia kile alichosema bila kuongeza tafsiri ambazo hakuzitoa.

Kauli hiyo ya Esma imekuja huku Diamond mwenyewe aliwahi kutoa kauli tofauti kuhusu idadi ya watoto wake. Januari mwaka 2021, katika mahojiano na Wasafi TV, Diamond amesema ana watoto sita, kauli iliyowashangaza baadhi ya mashabiki ambao walikuwa wakifahamu zaidi watoto wake waliokuwa wakionekana hadharani.

Wakati huo, watoto waliokuwa wakifahamika zaidi kwa umma ni Tiffah na Nillan ambao ni watoto wake na Zari Hassan, Naseeb Junior ambaye ni mtoto wake na Tanasha Donna, pamoja na Dylan ambaye ni mtoto wake na Hamisa Mobetto. Akizungumzia watoto wengine wawili aliowataja, Diamond amesema:

“Mmoja yupo mkoani Mwanza ambaye mama yake amegoma kunipatia, wa pili aliletwa na mama yake na nilimwona.”

Tofauti ya kauli hizo mbili za ndugu hao imeendelea kuwafanya baadhi ya mashabiki kujiuliza kuhusu idadi ya watoto wa Diamond, lakini kwa upande wake, Esma amesisitiza hakutoa maana mtoto fulani si wa kaka yake. Amesema alichozungumza ni tofauti na tafsiri ambazo zimeanza kusambaa mitandaoni.

Mbappe Wa Zanzibar Asaini Singida Black Stars Jannik Sinner Atwaa Ubingwa Wa Wimbledon