Jannik Sinner Atwaa Ubingwa Wa Wimbledon
LONDON, ENGLAND: KUNA wakati unaweza kuendelea kupiga mpira ukigonga ukuta mara nyingi, lakini mwisho ukajikuta unatamani kuupiga kichwa ukuta huo kwa hasira. Ndivyo ilivyokuwa kwa Alexander Zverev, ambaye alijikuta akiumizwa tena na ubora wa Jannik Sinner, aliyefanikiwa kutetea taji la Wimbledon kwa mara nyingine.
Alianzisha ‘servis’ kali zisizozuilika, hata aliwahi kuwa mbele katika mchezo. Lakini mbele yake alikutana na “ukuta” usiotikisika.
Ukuta unasimama imara. Ukuta hurudisha kila mpira. Na ndivyo alivyofanya Sinner.
Akiwa mtulivu na mwenye ubora wa hali ya juu, Sinner aligeuza mwelekeo wa mchezo na kuibuka mshindi kwa seti 6-7, 7-6, 6-3, 6-4, akitwaa taji lake la tano la Grand Slam.
Katika mchezo mzima, Muitaliano huyo hakuonyesha hisia nyingi wala mbwembwe, lakini alionyesha uimara wa kipekee. Zverev alipata nafasi moja tu ya break katika mechi nzima, lakini hata hiyo Sinner aliifanikiwa kuiokoa.
Kulikuwa na dalili zinazomkumbusha Novak Djokovic katika namna Sinner alivyochukua presha ya Zverev kwenye seti mbili za kwanza kabla ya kuanza kuutawala mchezo taratibu, akimchosha mpinzani wake hatua kwa hatua hadi kumaliza kazi.
Huenda haikuwa fainali ya kuvutia zaidi kwa upande wa burudani, lakini Sinner ameendelea kuthibitisha kuwa ushindi hauhitaji maonyesho makubwa, bali uthabiti na ubora.
Akiwa na umri wa miaka 24 pekee, tayari ameijengea historia kubwa taaluma yake kwa kutwaa Grand Slam tano.
“Ninajisikia vizuri sana. Kwanza kabisa nataka kumpongeza Sascha (Zverev). Leo ulikuwa karibu sana kushinda. Ukiendelea kucheza kwa kiwango hiki, nina uhakika na wewe utainua moja ya mataji haya siku moja.”
Kisha akaongeza kwa utani:
“Najua pia ndoto yako nyingine ni kuwa namba moja duniani. Upo karibu sana, hivyo tunapaswa kuwa makini.”
Mashabiki waliokuwa Centre Court walimshangilia kwa nguvu, lakini bado swali linaendelea kubaki; je, Sinner ataweza kupata mapenzi makubwa kutoka kwa mashabiki kama walivyowahi kupata Roger Federer, Rafael Nadal au Novak Djokovic?
Sinner hana uchezaji wa kifahari kama Federer. Haonyeshi hisia nyingi kama Nadal au Djokovic. Wala hana ubunifu wa kusisimua kama Carlos Alcaraz.
Badala yake, silaha zake ni kasi ya ajabu ya miguu, uwezo wa kubadili haraka kutoka kujilinda kwenda kushambulia, akili kubwa ya mchezo na utulivu wa hali ya juu katika nyakati zenye presha.
Ndiyo maana, hata alipochelewa pointi 2-0 kwenye tie-break ya seti ya pili, hakuyumba. Alirejea kwa nguvu na kuigeuza hali hiyo kuwa mwanzo wa ushindi wake.