Baada Ya kuwindwa Na Simba, Yona Achagua Singida Black Stars
KIPA mzawa, Yona Amos, amejiunga rasmi na Singida Black Stars kwa kusaini mkataba wa miaka miwili baada ya kumaliza mkataba wake na Pamba Jiji FC, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa klabu hiyo kuimarisha kikosi kuelekea msimu wa 2026/27.
Yona ametua Singida Black Stars kama mchezaji huru, akihitimisha safari yake ndani ya Pamba Jiji ambako alikuwa miongoni mwa makipa waliokuwa wakitegemewa kutokana na uwezo wake wa kulinda lango na kutoa mchango mkubwa kwa timu hiyo.
Baada ya kukamilisha taratibu zote za usajili, kipa huyo tayari amewasili kambini Singida na kuanza kuungana na wachezaji wenzake katika maandalizi ya msimu mpya, huku akitarajiwa kuanza mazoezi mara moja.
Kabla ya kutua Singida Black Stars, Yona aliwahi kuhusishwa na Simba, ambayo ilitajwa kuonyesha nia ya kumsajili ili kuongeza ushindani katika nafasi ya kipa, hasa baada ya Yakubu Seleman kukumbwa na majeraha.
Usajili wa Yona unatarajiwa kuongeza ushindani mkubwa katika eneo la golikipa ndani ya Singida Black Stars, ambayo imeendelea kufanya maboresho ya kikosi kwa lengo la kuwa na timu imara itakayoshindania nafasi za juu katika Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mashindano mengine ya ndani.
Kwa uzoefu alioupata akiwa Pamba Jiji, Yona anatarajiwa kuwa nguzo muhimu ya safu ya ulinzi ya Singida Black Stars na kusaidia timu hiyo kufikia malengo yake katika msimu ujao.
Akizungumzia usajili huo, Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Masanza, alisema klabu hiyo ilikuwa na mpango wa kuongeza kipa mmoja katika kikosi kama sehemu ya maboresho yanayoendelea kuelekea msimu mpya.