Yanga SC

Mwamnyeto Afunguka Yanga, Aacha Sintofahamu Kuhusu Hatma Yake

Vardo July 16, 2026 5:06 pm

NAHODHA wa Yanga SC, Bakari Mwamnyeto, ameutaja msimu uliomalizika wa Ligi Kuu ya NBC kuwa ulikuwa wa kipekee na wenye mafanikio makubwa, huku akiacha maswali kuhusu hatma ya maisha yake ya soka ndani ya klabu hiyo.

Mwamnyeto, ambaye alikuwa sehemu muhimu ya safari ya Yanga kutwaa ubingwa wa ligi kwa mara ya tano mfululizo, amesema msimu huo ulikuwa wa kipekee kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo katika kila mchezo.

Beki huyo ameuita msimu huo kuwa wa “kiume”, akieleza kuwa kila timu ilipambana kwa nguvu kuhakikisha inapata matokeo, jambo lililowafanya wao kuongeza umakini na kujituma zaidi hadi kufikia lengo lao.

Akikumbuka safari ya ubingwa huo, Mwamnyeto alitaja mchezo dhidi ya Dodoma Jiji FC kuwa moja ya mechi ngumu na za kihistoria kwake, akisema ulikuwa mtihani mkubwa ambao ungeweza kubadili mwelekeo wa mbio za ubingwa.

“Ulikuwa mchezo uliojaa makosa mengi ambayo yangeweza kubadili kila kitu na kupoteza mwelekeo wetu. Lakini kwa neema ya Mungu, mwisho wa safari ukawa wa furaha kubwa. Nilichojifunza ni kwamba kilichoandikwa na Mungu hakizuiliki,” amesema Mwamnyeto.
Hata hivyo, kuhusu mustakabali wake ndani ya Yanga huku mkataba wake ukiwa moja ya mambo yanayozungumziwa, nahodha huyo ameonekana kuwa makini na suala hilo, akisisitiza kuwa bado si wakati wa kutoa uamuzi wa mwisho.

Mwamnyeto amesema kwa sasa ni mapema kuzungumzia iwapo ataendelea kubaki Jangwani au kuangalia changamoto mpya nje ya klabu hiyo, akitaka muda zaidi kabla ya kuweka wazi hatua yake inayofuata.

Kauli hiyo imeacha mashabiki wa Yanga wakisubiri kwa hamu hatma ya nahodha huyo ambaye amekuwa nguzo muhimu katika mafanikio ya klabu hiyo katika misimu ya hivi karibuni.

Skudu Astaafu Kucheza Soka, Kituo Kinachofuata Ukocha JKT Tanzania Yamnasa Malimi Baada Ya Kukosa Dili La Simba