Simba Yaaga nNyota Saba, Yafungua Ukurasa Mpya Kuelekea Msimu Wa 2026/27
KLABU ya Simba SC imetangaza rasmi kuachana na wachezaji saba ikiwa ni sehemu ya mpango wa kufanya maboresho ya kikosi kuelekea msimu wa 2026/27.
Uamuzi huo unaonyesha dhamira ya klabu kujenga timu yenye ushindani mkubwa kwa ajili ya mashindano ya ndani na kimataifa.
Wachezaji watano kati ya walioondoka walikuwa wakiitumikia Simba kwa mikataba ya mkopo. Hao ni Omari Omari aliyekuwa ametokea Mashujaa FC, Joshua Mutale kutoka Al-Adalah ya Saudi Arabia, Chamou Karaboue wa TRA United, Awesu Awesu kutoka Polisi Kenya na Edwin Balua aliyekuwa ametokea Al Entisar ya Saudi Arabia.
Mbali na kundi hilo, Simba pia imehitimisha ushirikiano wake na nyota wawili raia wa Guinea, kiungo Naby Camara na kipa Moussa Camara.
Moussa alikumbwa na majeraha ya muda mrefu yaliyomuweka nje ya uwanja kwa kipindi kikubwa cha msimu uliopita, jambo lililoathiri mchango wake ndani ya kikosi.
Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na klabu hiyo, Simba imewashukuru wachezaji wote walioondoka kwa kujitolea na mchango wao wakiwa sehemu ya kikosi, huku ikiwatakia mafanikio mema katika hatua inayofuata ya maisha yao ya soka.
Kuondoka kwa wachezaji hao kunafungua nafasi kwa uongozi wa Simba kuendelea na mchakato wa kukisuka kikosi kipya kitakachokuwa na ushindani mkubwa katika Ligi Kuu ya NBC, Kombe la Shirikisho la CRDB pamoja na mashindano ya kimataifa msimu ujao.
Wakati huo huo, mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi wanasubiri kwa hamu kutambulishwa kwa nyota wapya watakaoziba nafasi za walioondoka, huku uongozi ukiendelea kukamilisha mipango ya kuimarisha kikosi kabla ya kuanza rasmi maandalizi ya msimu wa 2026/27.