Kiungo Yanga Aibukia Singida
TAARIFA kutoka Singida Black Stars, zinabainisha kwamba, kiungo wa kati wa Yanga, Shekhani Khamis, tayari ameshaanza mazoezi na kikosi hicho alichojiunga nacho kwa mkopo wa msimu mmoja wa 2026-2027, hatua hiyo imekujaa baada ya kukosa nafasi kubwa ya kucheza kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu ya NBC.
Kwa Singida BS ushindani ambao atakutana nao wa namba ni dhidi ya Ahmed Pipino, Linda Mtange, Khalid Habib Idd ‘Gego’ huku Khalid Aucho ikielezwa hataendelea kukichezea kikosi hicho.
Ukiachana na Shekhan, mwingine aliyeanza mazoezi na Singida Black Stars baada ya kusajiliwa kwa mkataba wa miaka mitatu ni kipa Yona Amosi aliyetoka Pamba Jiji ambaye msimu wa 2025-2026 alimaliza akiwa na cleansheets nane za Ligi Kuu ya NBC na 2024-2025 alikuwa na cleansheets 11.
Wakati huohuo, taarifa za mshambuliaji Jonathan Sowah raia wa Ghana kurejea Singida Black Stars akitangazwa kuitumikia timu hiyo kuanzia 2026 hadi 2029, zimepokewa vizuri na kocha wa kikosi hicho, Muhibu Kanu.