Mngqithi Atua Bongo, Yanga Kujichimbia Avic Town Kuiwinda Simba Ngao ya Jamii.
Shauku ya mashabiki wa Yanga SC kutaka kuona kikosi chao kipya cha msimu ujao inakaribia kutimia, kwani klabu hiyo imetangaza rasmi kuanza maandalizi yake siku ya Jumatatu, Julai 20, 2026.
Kuelekea kambi hiyo, kocha mkuu mpya wa Wananchi, Manqoba Mngqithi, alitarajiwa kutua nchini usiku wa kuamkia leo akitokea nchini kwao Afrika Kusini. Mngqithi anawasili akiambatana na wasaidizi wake watatu tayari kwa kuunda benchi jipya la ufundi, huku akiendelea kufanya kazi na baadhi ya wataalam waliokuwepo kwenye benchi lililopita.
Kambi Kuwa Avic Town Kigamboni
Kufuatia kufutiliwa mbali kwa mpango wa kwenda kuweka kambi nchini Afrika Kusini na kushiriki michuano ya Toyota, Yanga sasa itajichimbia hapahapa nchini. Kikosi hicho kitaweka ngome yake katika kituo chao cha kisasa cha Avic Town kilichopo Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Kituo hicho kimefanyiwa maboresho makubwa hivi karibuni, ikiwemo ujenzi wa Gym ya kisasa itakayotumika kwa ajili ya mazoezi ya viungo, hatua inayoondoa ulazima wa timu hiyo kwenda viwanja vya Gymkhana kama ilivyokuwa awali. Avic Town imeipa Yanga mafanikio makubwa kwani wamewahi kujiandaa hapo na kufanikiwa kutwaa mataji matatu kati ya matano mfululizo.
Usiri na Ulinzi Mkali Watawala
Katika kuhakikisha mbinu na silaha zao mpya hazivuji, uongozi wa Yanga umepanga kuweka ulinzi mkali sana kambini hapo.
Kiongozi mmoja mwandamizi wa klabu hiyo ameeleza kuwa hakuna mtu yeyote, nje ya viongozi, atakayeruhusiwa kushuhudia mazoezi hayo. Hata mechi za kirafiki za kujipima nguvu zitachezwa hapohapo kambini kwa usiri mkubwa, na mashabiki watahitajika kusubiri siku ya mechi uwanjani ndipo waone makali ya timu yao.
Kuelekea Ngao ya Jamii
Yanga, ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya NBC, wataanza rasmi kampeni yao ya kutetea mataji kwa kuwavaa watani wao wa jadi, Simba SC, katika mchezo wa Ngao ya Jamii unaotarajiwa kupigwa Agosti 12, 2026.
Wakati Yanga wakijichimbia Kigamboni, wapinzani wao Simba SC wanatarajiwa kuingia kambini kuanzia Jumamosi ya Julai 18, 2026, wakijiandaa na safari ya kuelekea nchini Rwanda kushiriki michuano ya Kombe la Kagame itakayotimua vumbi kuanzia Julai 24 hadi Agosti 7, 2026.