Usajili Simba SC 2026/27
Simba SC

Usajili Simba SC 2026/27: Mwalimu Asaini Miaka Miwili, Oura Abaki, Hawa Hapa Walioachwa!

admin July 17, 2026 11:17 am

Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, ameanza kusuka kikosi chake cha mauaji kuelekea msimu wa 2026-2027, huku kipaumbele chake cha kwanza kikiwa ni kubakisha nyota muhimu walioipa mafanikio timu hiyo.

Barker, ambaye ameiongoza Simba kutwaa Kombe la Shirikisho la CRDB na Kombe la Muungano tangu akabidhiwe mikoba Desemba 2025, tayari ametoa mapendekezo ya nani abaki na nani aondoke.

Mwalimu Asaini Miaka Miwili

Taarifa njema kwa Wanasimba ni kwamba, mshambuliaji wao kinara msimu uliopita, Seleman Mwalimu, ataendelea kusalia Msimbazi. Uongozi wa Simba umefikia makubaliano ya kumnunua moja kwa moja mshambuliaji huyo kutoka Wydad AC ya Morocco, akisaini mkataba wa miaka miwili utakaomuweka klabuni hapo hadi msimu wa 2027-2028.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeeleza kuwa: “Awali ilitakiwa tukae mezani na Wydad baada ya mkopo kuisha, lakini kocha alituambia Mwalimu ameshaingia kwenye mfumo wake na anamhitaji. Hivyo tumekubaliana na Wydad kumchukua moja kwa moja.”

Mwalimu (20) alimaliza msimu wa 2025-2026 kama kinara wa mabao ndani ya Simba akifunga mabao tisa (9) kwenye Ligi Kuu, akifuatiwa na Clatous Chama mwenye mabao manane (8). Thamani yake sokoni kwa sasa inakadiriwa kufikia Euro 150,000 (zaidi ya Sh452 Milioni).

Oura Abaki, Makgalwa Ndani

Kama ilivyoripotiwa awali, kiungo mshambuliaji Anicet Oura haendi popote. Licha ya kuwepo kwa ofa tatu kutoka Ulaya, Kocha Barker ameshikilia msimamo wa kumbakisha raia huyo wa Ivory Coast. Hatua hii inakuja wakati Simba ikikamilisha usajili wa winga raia wa Afrika Kusini, Keletso Makgalwa, akitokea Sekhukhune United.

Hata hivyo, hatima ya kiungo Neo Maema, aliyecheza kwa mkopo kutoka Mamelodi Sundowns, bado inasubiri majibu. Kocha anamtaka, lakini uongozi bado unaendelea na mazungumzo.

Ishu ya Golini na Majeruhi

Kwenye idara ya ulinzi langoni, Barker amependekeza kipa Djibrilla Kassali aendelee kusalia. Kipa huyo amechukua nafasi ya Moussa Camara, ambaye mkataba wake umemalizika baada ya kukaa nje msimu mzima wa 2025-2026 kutokana na majeraha. Hussein Abel anatajwa kuwa njiani kuondoka, huku Yakoub Suleiman akiendelea kujiuguza baada ya kufanyiwa upasuaji.

Nyota Saba (7) Waonyeshwa Mlango wa Kutokea

Ili kupata nafasi ya kuingiza damu mpya, mchana wa jana Simba SC ilitangaza rasmi kuachana na wachezaji wake saba (7) ambao hawatakuwa sehemu ya mipango ya msimu ujao. Wachezaji walioagwa ni:

Chamou Karaboue

Naby Camara

Edwin Balua

Joshua Mutale

Awesu Awesu

Omari Omari

Moussa Camara

Kwa hatua hizi, ni wazi kuwa Simba SC imedhamiria kufanya kufuru kwenye soko la usajili ili kuendeleza ubabe wake baada ya kufunga msimu wa 2025-2026 kwa kishindo kwa kuwafunga Azam FC na Yanga SC na kubeba mataji mawili muhimu.

Kiungo Yanga Aibukia Singida Siri ya Picha ya Lamine Yamal Alipokuwa Mtoto Mikononi Mwa Messi.