Miaka 11 Bila Banza Stone: Urithi Na Kilio Cha Familia Ya Maestro Wa Dansi
Julai 17, 2026, ilitimia miaka 11 tangu kufariki kwa mmoja wa waimbaji mahiri na magwiji wa muziki wa dansi nchini Tanzania, Ramadhani Masanja, maarufu kama Banza Stone. Alifariki dunia mwaka 2015 baada ya kuugua kwa muda mrefu. Ingawa ni muongo mmoja na ushee umepita, kazi zake bado zinaendelea kutikisa kwenye redio, majukwaa ya kidijitali, na kubaki kwenye nyoyo za mashabiki.
Banza Stone alikuwa na sauti ya kipekee, uwezo mkubwa wa kutunga mashairi, na ujumbe wenye mafunzo mazito. Nyimbo zake kama Mtaji wa Maskini, Kumekucha, Elimu ya Mjinga, Angurumapo Simba, Mtu Pesa, na Falsafa ya Maisha zilimjengea heshima kubwa katika tasnia ya muziki wa Tanzania.
Safari Yake ya Muziki Ilianzia Utotoni
Banza Stone alizaliwa Oktoba 20, 1972, jijini Dar es Salaam. Baada ya kumaliza elimu ya msingi, mapenzi yake kwa muziki yalimvutia kujiunga na vikundi mbalimbali vya burudani, ingawa wazazi wake mwanzoni hawakuunga mkono uamuzi huo.
Alianza kwa kujaribu muziki wa Hip Hop kabla ya kuamua kuelekeza nguvu zake zote katika muziki wa dansi. Pia alipata mafunzo ya muziki katika Jumba la Utamaduni la Korea, hatua iliyomsaidia sana kujenga taaluma na misingi imara ya muziki wake.
Njia Alizopita Kabla ya Kung’ara
Kabla ya kuwa nyota mkubwa, Banza Stone alipitia bendi mbalimbali zikiwemo The Heart Strings, Twiga Band, Achigo Band, na Afri-Swez, kabla ya kujiunga na African Stars Band ‘Twanga Pepeta‘, ambako kipaji chake kilianza kutambulika kwa kiwango cha juu kitaifa.
Baadaye alijiunga na TOT Plus, akarudi tena Twanga Pepeta, kisha Extra Bongo, huku pia akianzisha bendi yake ya Bambino Sound, ambayo hata hivyo haikudumu kwa muda mrefu. Safari hii ilimjengea uzoefu mkubwa na kumfanya kuwa mmoja wa waimbaji waliokuwa wakiheshimika zaidi.
Nyimbo Zilizooacha Historia
Kilichomtofautisha Banza Stone na wasanii wengine ni uwezo wake wa kuandika nyimbo zenye mafunzo ya maisha, mapenzi, na changamoto za jamii.
Wapenzi wa muziki wa dansi bado wanazikumbuka kazi zake ngumu kusahaulika kama Mtaji wa Maskini, Elimu ya Mjinga, Kumekucha, Angurumapo Simba, Mtu Pesa, Falsafa ya Maisha, Hujafa Hujasifiwa, Jahazi, na Euro ambazo hadi leo zimekuwa nguzo kwenye vipindi vya burudani.
Dakika za Mwisho na Kifo Kilichoacha Simanzi
Katika miezi ya mwisho ya maisha yake, afya ya Banza Stone ilianza kudhoofika sana kutokana na ugonjwa uliomfanya ashindwe kutembea au kujihudumia mwenyewe. Baada ya uvumi mwingi wa mitandaoni, hatimaye Julai 17, 2015, alifariki dunia nyumbani kwao Sinza Kijiweni, Dar es Salaam. Mazishi yake yalifanyika Julai 18, 2015, katika makaburi ya Sinza na kuhudhuriwa na mamia ya waombolezaji.
Kauli ya Familia: Tunaishi kwa Upweke
Katika kuadhimisha miaka 11 ya kumbukumbu yake, kaka wa marehemu, Hassan Masanja, alieleza kuwa familia iliandaa dua maalumu nyumbani kwao Sinza. Hata hivyo, Hassan alieleza masikitiko yake kuhusu kukosekana kwa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya wanamuziki na viongozi wa bendi waliokuwa karibu na Banza enzi za uhai wake.
“Leo (Julai 17) hatuna shughuli kubwa zaidi ya dua ya kumuombea Banza nyumbani. Kila mwaka familia hukutana kumkumbuka. Lakini ukweli ni kwamba tangu Banza afariki, mawasiliano na wengi wa wanamuziki aliowahi kufanya nao kazi yamekuwa hafifu, jambo linalotuwacha tukiwa na upweke,” alisema Hassan.
Wanamuziki Watoa Kauli zao
Akijibu mtazamo huo, kiongozi wa Twanga Pepeta, Luizer Mbutu, alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo lakini akasema ni kawaida kwa jamii yetu:
“Ni kweli kabisa, mawasiliano hayapo kama alipokuwa hai. Hii ni kawaida kwetu Watanzania, si kwa Banza tu. Mimi siku Mungu akinichukua, familia yangu huenda isiwe na mawasiliano na watu wangu wa karibu kwa sababu mimi ndiye niliyekuwa kiunganishi.”
Kwa upande wake, Ramadhani Mhoza ‘Rama Pentagone’, alibainisha kuwa familia haikuwa karibu sana na wanamuziki wakati msanii huyo yuko hai, tofauti na mama yake mzazi ambaye alikuwa nguzo na kiungo kati ya wasanii na familia.
Urithi Wake Bado Unaishi
Hata hivyo, wanamuziki wote walikubaliana kuwa mchango wa Banza Stone hauwezi kufutika. Alikuwa msanii wa kipekee—mwimbaji, mtunzi, na mpiga ngoma mahiri aliyetumia sanaa yake kuelimisha jamii badala ya kuimba burudani ya mapenzi pekee. Miaka 11 baadaye, kazi zake thabiti zinathibitisha msemo wa kale: “Wasanii hufa, lakini kazi zao huishi milele.”