Arobaini ya mtoto wa Wema Sepetu
Michezo Bongo

Wema Sepetu Afunguka Kuhusu Viingilio Vya Sherehe Ya Mtoto Wake Ollie

Vardo July 18, 2026 10:07 pm

DAR ES SALAAM: Baada ya kutangaza viingilio vya sherehe ya arobaini ya mtoto wake, Ollie, muigizaji na Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu, amefafanua kuhusu bei hizo ambazo zimezua mjadala mkubwa kwa baadhi ya mashabiki wake mitandaoni.

Wema ametangaza kuwa, sherehe hiyo ya kumshukuru Mungu kwa hatua ya siku 40 ya mtoto wake itafanyika Julai 23, 2026 katika ukumbi wa The SuperDome, Masaki jijini Dar es Salaam.

Tangazo la viingilio hivyo limeibua maoni mbalimbali, hasa baada ya kufahamika kuwa kifurushi cha juu zaidi cha kushiriki tukio hilo kinafikia Sh5 milioni. Baadhi ya mashabiki wameona kiwango hicho ni kikubwa mno kwa tukio linalohusisha mtoto wa msanii mwenye mashabiki wengi wa hali ya chini na kati.

Wema Sepetu Ajibu Malalamiko ya Mashabiki

Akizungumza na Soka La Bongo, Wema Sepetu amesema hakuna tatizo katika viwango hivyo kwa sababu vimepangwa kwa namna ambayo kila mtu ataweza kushiriki kulingana na uwezo wake wa kifedha.

Wema amefafanua kuwa ndiyo maana wameweka bei tofauti tofauti, ili kila anayetamani kuwa sehemu ya tukio hilo la kihistoria aweze kuchagua kiwango kinachomfaa bila kuumia.

Acha iwe hivyo jamani, mbona hakuna shida. Kuna bei tofauti tofauti, kila mtu ataingia sehemu ambayo uwezo wake unamruhusu. Nawapenda mashabiki zangu na natamani siku hiyo wajitokeze kwa wingi kufurahia kwa pamoja, wasilalamike sana jamani, waje tu,” amesema Wema.

Safari ya Wema na Whozu Kupata Mtoto

Sherehe hiyo inakuja baada ya Wema na mchumba wake, mwanamuziki Whozu, kupata mtoto wao wa kwanza, Ollie, ambaye amekuwa gumzo kubwa tangu kuzaliwa kwake kutokana na umaarufu wa wazazi wake katika tasnia ya burudani ya Bongo.

Juni 23, 2026, Wema alijifungua mtoto huyo, tukio ambalo lilipokewa kwa furaha na nderemo kubwa na mashabiki wake baada ya safari ndefu na ya changamoto ya kusubiri kupata mtoto.

Kabla ya sherehe hii ya arobaini, Julai 16, 2026, familia hiyo ilifanya pia hafla ya Akika ya Ollie, iliyofanyika nyumbani kwa mama mzazi wa Wema Sepetu eneo la Sinza jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kumshukuru Mungu kwa mtoto huyo kuzaliwa salama.

Mchanganuo wa Viingilio

Kwa mujibu wa tangazo la Wema, viingilio vya sherehe ya Julai 23 vimepangwa katika viwango vifuatavyo:

  • Sh 100,000

  • Sh 300,000

  • Sh 500,000

  • Sh 5,000,000 (V.I.P / Huduma Maalumu)

Tangu kutangazwa kwa viingilio hivyo, mitandao imechafuka kwa maoni tofauti, huku wengine wakisema ni gharama kubwa mno na wengine wakisisitiza kuwa ni uamuzi wa familia kuweka viwango wanavyoona vinafaa kwa hadhi ya tukio lao.

Hata hivyo, Wema anaonekana kusimama imara na mpangilio huo akisisitiza kuwa lengo ni kumpa kila mtu nafasi ya kushiriki kwa kiwango anachoweza, huku maandalizi ya sherehe hiyo yakitarajiwa kuwa miongoni mwa matukio makubwa ya burudani yatayokusanya mastaa wengi jijini Dar es Salaam.

Mixx Super App Kutoa Milioni 50 Tamati Ya Kombe La Dunia 2026 Miaka 11 Bila Banza Stone: Urithi Na Kilio Cha Familia Ya Maestro Wa Dansi