Ahoua Kutua Singida Black Stars: Usajili wa Ahoua na Mipango ya Cecafa
Ni suala la muda tu kabla ya Singida Black Stars kukamilisha usajili wa aliyekuwa kiungo mshambuliaji machachari wa Simba SC, Jean Charles Ahoua, ili kuimarisha kikosi chao kuelekea msimu ujao wa mashindano.
Ahoua, ambaye alionyesha kiwango cha juu alipokuwa akicheza Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024-2025 na kuibuka mfungaji bora akiwa na mabao 16 na asisti tisa, alitimkia klabu ya CR Belouizdad ya Algeria wakati wa dirisha dogo la usajili Januari 2026. Hata hivyo, baada ya kudumu nchini Algeria kwa takribani miezi sita, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 anatajwa kurejea kwenye soka la Bongo.
Kuungana na Timu Rwanda (Cecafa Kagame Cup)
Taarifa za ndani kutoka kwa mmoja wa viongozi wa juu wa Singida Black Stars zinaeleza kuwa mchakato wa usajili huo umefikia hatua nzuri. Kuna uwezekano mkubwa nyota huyo akajiunga na wenzake nchini Rwanda, ambako klabu hiyo inashiriki michuano ya Cecafa Kagame Cup 2026 kama bingwa mtetezi.
“Kuna wachezaji wengi wapya tuliowasajili ambao wataungana na timu nchini Rwanda. Kwa kuwa tunakwenda kutetea ubingwa wetu wa Cecafa Kagame Cup, suala la Ahoua likikamilika mara moja ataungana na wenzake huko,” alisema kiongozi huyo.
Mosi Nduwumwe Kuuzwa, Jonathan Sowah Arejea
Wakati usajili wa Ahoua ukiiva, taarifa nyingine zinabainisha kuwa Singida Black Stars ipo mbioni kumuuza mshambuliaji wake hatari, Mosi Nduwumwe, aliyeibuka kinara wa ufungaji Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025-2026 akipachika mabao 17 (ikiwemo hat-trick mbili).
Akiungumzia mipango ya safu ya ushambuliaji, kiongozi huyo aliongeza kuwa klabu hiyo pia imemrejesha mshambuliaji Jonathan Sowah ili kuongeza nguvu.
Sowah alionyesha uwezo mkubwa katika msimu wake wa kwanza (2024-2025) akifunga mabao 13, kabla ya kujiunga na Simba msimu wa 2025-2026 ambapo alipachika mabao matatu licha ya kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara. Uongozi unaamini mchanganyiko wa Ahoua na Sowah utatengeneza safu ya ushambuliaji yenye ushindani mkubwa msimu ujao.