Fainali ya CECAFA Kagame Cup 2026
Michezo Bongo

Fainali CECAFA 2026: Vita ya Kagere na Niyonzima Gor Mahia vs Rayon Sports

Vardo August 7, 2026 10:24 am

Kuna msemo maarufu nchini Rwanda unaosema ‘Umutima ntushobora gukunda impande ebyiri icyarimwe’—moyo hauwezi kupenda pande mbili kwa wakati mmoja. Msemo huu unajidhihirisha wazi kwa mastaa wawili wa zamani wa Timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi), Meddie Kagere na Haruna Niyonzima, saa chache kabla ya pambano la kukata na shoka la Fainali ya CECAFA Kagame Cup 2026.

Leo Ijumaa, macho na masikio ya wapendasoka wote Afrika Mashariki yatakuwa kwenye Uwanja wa Amahoro, jijini Kigali. Ni vita ya kusaka bingwa mpya wa ukanda huu kati ya Rayon Sports ya Rwanda na Gor Mahia ya Kenya, baada ya Al Hilal ya Sudan na Jamus za nchini Sudan Kusini kuwania nafasi ya tatu.

Nje ya uwanja, kuna ‘bato’ lingine la aina yake kati ya Kagere na Niyonzima—mastaa waliowahi kuandika historia kubwa kwenye soka la ukanda huu, ambapo sasa kila mmoja ana sababu za msingi za kuitakia ushindi timu yake ya moyoni.


Kagere: Moyo Wangu Uko Gor Mahia

Kwa mashabiki wa Gor Mahia (K’Ogalo), jina la Meddie Kagere halihitaji utambulisho. Alipotua Nairobi mwaka 2015, aligeuka kivutio na kuwa mmoja wa washambuliaji hatari zaidi kwenye Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

Akiwa na Gor Mahia kati ya mwaka 2015 na 2018, Kagere alipachika mabao 50 katika mashindano yote—takwimu zinazomweka kwenye orodha ya wafungaji 10 bora wa muda wote wa klabu hiyo. Mbali na mabao, aliisaidia Gor Mahia kutwaa mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu (2015, 2017, 2018), huku pia akitwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka (SJAK MVP) mwaka 2017.

Akizungumzia fainali ya leo, mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba SC alikiri kuwa pambano litakuwa gumu lakini mapenzi yake yako Kenya.

“Gor Mahia ni sehemu kubwa ya maisha yangu ya soka. Nilipata mafanikio makubwa pale, nilishinda mataji na kupata upendo mkubwa kutoka kwa mashabiki. Ni halali moyo wangu uwe upande wao leo,” alisema Kagere.

Hata hivyo, Kagere aliongeza kuwa Rayon Sports ni timu hatari inapocheza nyumbani kwenye Uwanja wa Amahoro, lakini uzoefu wa Gor Mahia kwenye mechi kubwa utamua mchezo huo.


Haruna Niyonzima: Rayon Sports lazima Ibakishe Kombe Nyumbani

Upande wa pili yupo kiungo maestro, Haruna Niyonzima. Kabla ya kutamba na klabu za APR, Yanga SC, Simba SC na kuwa nahodha wa muda mrefu wa Amavubi (akicheza mechi 112 za kimataifa), safari yake ilianzia Rayon Sports kati ya mwaka 2006 na 2007.

Ingawa alipata mafanikio makubwa baadaye, Niyonzima hajawahi kuficha mapenzi yake kwa Rayon Sports—klabu iliyomfungulia milango ya soka la ushindani.

“Ni mchezo mkubwa mno. Gor Mahia wana historia na uzoefu, lakini Rayon Sports ina kila sababu ya kujiamini. Wamefika fainali kwa kiwango cha juu na wanacheza nyumbani mbele ya mashabiki wao,” alisema Niyonzima.

Kiungo huyo wa zamani amewataka wachezaji wa Rayon Sports kutuliza presha na kutumia vyema fursa ya kushangiliwa na mashabiki wao ili kubakiza taji hilo nchini Rwanda.


Njia za Timu Hizi Kuelekea Fainali

Njia ya kuelekea fainali haikuwa rahisi kwa timu zote mbili:

  • Gor Mahia (Kundi A): Njia yao ilianza kwa ushindi mnono wa 5-0 dhidi ya APR, kabla ya kuchapwa 1-0 na Vipers. Walizinduka na kuichapa Garde Republicaine ya Djibouti 1-0 na kutinga nusu fainali kwa wastani mzuri wa mabao kabla ya kuing’oa Al Hilal.

  • Rayon Sports (Kundi C): Walitinga hatua ya mtoano kwa rekodi ya kishindo baada ya kushinda mechi zote za makundi—wakiwachapa KVZ (2-0), Tusker FC (1-0), na Al Hilal (1-0), kisha wakaiondoa Jamus kwenye nusu fainali.


Mbio za Dola 30,000 za Marekani

Mbali na heshima na historia ya kutwaa Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, fainali ya leo inabeba msisimko wa fedha taslimu:

  1. Mshindi wa Kwanza (Bingwa): Dola 30,000 za Marekani (Zaidi ya Tsh Milioni 75+)

  2. Mshindi wa Pili: Dola 20,000 za Marekani

  3. Mshindi wa Tatu: Dola 10,000 za Marekani

Mchezo huu wa Fainali utapigwa rasmi leo Ijumaa majira ya saa 2:00 Usiku (Kwa saa za Afrika Mashariki / Tanzania). Je, ni Rayon Sports watakaobakiza kombe nyumbani au Gor Mahia watavuka mpaka na taji hilo kwenda Nairobi?

Stand United Yaweka Wazi Mipango ya Usajili na Kambi: Watamba Kurejea Upya Championship! Mossi Nduwumwe Ajiunga MC Alger, Aweka Rekodi Mpya Akiondoka Singida Black Stars