Mossi Nduwumwe kujiunga MC Alger
Michezo Bongo

Mossi Nduwumwe Ajiunga MC Alger, Aweka Rekodi Mpya Akiondoka Singida Black Stars

Vardo August 7, 2026 10:32 am

Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Mossi Nduwumwe, amekamilisha rasmi uhamisho wake kutoka klabu ya Singida Black Stars na kujiunga na mabingwa wa soka nchini Algeria, MC Alger.

Uhamisho huu unahitimisha tetesi za muda mrefu zilizokuwa zikimhusisha nyota huyo na vilabu mbalimbali barani Afrika, kufuatia kiwango chake bora alichoonyesha katika msimu uliopita ndani ya Ligi Kuu ya NBC nchini Tanzania.

Klabu ya MC Alger imemthibitisha mchezaji huyo rasmi kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii kwa ujumbe mfupi wa kuwakaribisha mashabiki: “Welcome to Mouloudia”, ikiwa ni ishara ya kumalizika kwa mazungumzo na kukamilika kwa taratibu zote za usajili.

Rekodi ya Kipekee Ndani ya Ligi Kuu ya NBC

Mossi anaondoka Singida Black Stars akiwa ameacha alama kubwa nchini Tanzania. Licha ya kujiunga na timu hiyo mwezi Januari akitokea Flambeau du Centre FC ya Burundi na kucheza kwa nusu msimu pekee, aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kupachika mabao 17.

Katika kipindi hicho kifupi, Mossi aliweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyefunga hat-trick mbili katika msimu wa 2025/26. Mabao yake matatu dhidi ya Fountain Gate ndiyo yaliyomhakikishia kutwaa kiatu cha ufungaji bora na kumfanya kuvutia macho ya majitu ya soka barani Afrika.

Sababu ya Kutokuwepo Kwenye Pre-Season Rwanda

Kuondoka kwa Mossi kunatoa majibu ya kwanini mshambuliaji huyo hakuwepo kwenye kikosi cha Singida Black Stars kilichoweka kambi mjini Kigali, Rwanda, kujiandaa na msimu mpya pamoja na michuano ya CECAFA Kagame Cup. Wakati huo, mazungumzo ya kina kati ya viongozi wa Singida Black Stars na MC Alger yalikuwa yakiendelea kwa siri kubwa kabla ya kufikia muafaka.

Hivi sasa, Mossi anajiandaa kuanza changamoto mpya nchini Algeria ambapo ataungana na MC Alger katika kutetea ubingwa wao wa ndani pamoja na kushiriki Michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika (CAF Champions League) msimu ujao.

Fainali CECAFA 2026: Vita ya Kagere na Niyonzima Gor Mahia vs Rayon Sports Simba Yapeleka Ofa Wydad AC Kumsajili Selemani Mwalimu Jumla!