Maandalizi ya AFCON 2027: Serikali Yatoa Kauli Nzito Kuelekea Desemba 2026
DAR ES SALAAM: Serikali ya Tanzania imetoa ahadi nzito ikithibitisha kuwa kufikia Desemba 2026, maandalizi yote ya Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) yatakuwa yamekamilika kwa kati ya asilimia 90 hadi 100.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ameeleza kuwa ingawa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) limekuwa likifanya ukaguzi wa mara kwa mara, lengo kuu la Serikali ni kuhakikisha kila miundombinu inakuwa tayari kabla ya mwaka wa mashindano.
“Tunashukuru CAF kwa kuendelea kuonyesha imani kubwa kwetu katika maandalizi ya AFCON mwakani. Sisi kama Serikali tunataka hadi kufikia Desemba 2026, tumekamilisha kila kitu,” amesema Makonda.
Hatua ya Viwanja na Miundombinu
Waziri Makonda ameongeza kuwa viwanja vingi vitakavyotumika kwa ajili ya mechi rasmi pamoja na mazoezi vipo katika hatua nzuri ya ujenzi na ukarabati. Hatua hii inatoa matumaini makubwa kwa Watanzania na ukanda mzima wa Afrika Mashariki kuelekea mashindano hayo ya kihistoria.
Kazi hii inakuja huku Serikali ikiendelea kuwekeza fedha nyingi katika miundombinu ya michezo ili kuhakikisha Tanzania inawasilisha mashindano ya viwango vya juu zaidi barani Afrika.