Simba Queens Yaitambulisha Safu Mpya Simba Day: Mgosi Aongoza Jahazi!
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, Simba Queens, wameanza rasmi safari ya msimu mpya wa 2026/27 baada ya kutambulisha benchi lao jipya la ufundi pamoja na kikosi kamili cha wachezaji mbele ya maelfu ya mashabiki waliokiwa wamejitokeza katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Utambulisho huo ulikuwa miongoni mwa matukio yaliyovuta hisia za wengi katika kilele cha tamasha la Simba Day. Mshambuliaji wa zamani na nguli wa klabu hiyo, Mussa Hassan Mgosi, ametambulishwa rasmi kuwa Kocha Mkuu atakayeiongoza Simba Queens katika vita ya kusaka mataji msimu huu.
Baada ya utambulisho wa benchi la ufundi, zamu ilifuata kwa wachezaji watakaobeba jukumu la kuitetea nembo ya Simba Queens katika michuano ya ndani na kimataifa.
Macho Kwenye Michuano ya CECAFA na Afrika
Ikiwa inaingia msimu wa 2026/27 kama mfalme wa soka la wanawake nchini, Simba Queens imeweka wazi kuwa lengo lao kuu sio tu kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, bali pia kufanya vizuri kwenye michuano ya CECAFA.
Ushindi katika michuano ya CECAFA utawapa nafasi ya moja kwa moja ya kuiwakilisha kanda hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa Wanawake (CAF Women’s Champions League).
Ali Kiba Anogesha Kilele cha Simba Day
Nje ya dimba, tamasha hilo lilipata msisimko wa pekee baada ya msanii nguli wa muziki wa Bongo Flava, Ali Kiba, kupanda jukwaani na kutoa burudani ya kukatisha shoka iliyowashangaza na kuwalipua maelfu ya Wanasimba waliofurika uwanjani hapo.