Kocha Gaborone United Aivulia Kofia Yanga, Aweka Wazi Mbinu za Kuwashangaza Ligi ya Mabingwa
KOCHA wa Gaborone United, Sean Connor, amekiri kutambua ukubwa na ugumu wa kuikabili Yanga SC katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini amesisitiza kuwa wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na mkakati maalum wa kupata matokeo na kusonga mbele.
Connor, ambaye amewahi kuhudumu kama Mkurugenzi wa Ufundi wa Cape Town Spurs ya Afrika Kusini, amesema anaiheshimu Yanga inayofundishwa na Manqoba Mngqithi, lakini lengo lao kuu ni kufanya maajabu na kujirekebisha ili kutokurudia makosa yaliyowagharimu dhidi ya Simba SC msimu uliopita.
Yanga ni Timu Kubwa Afrika
Katika droo ya CAF, Gaborone United imepangwa kuanzia nyumbani Botswana kabla ya kusafiri kuja Tanzania kurudiana na Yanga. Akizungumzia mechi hiyo, Connor alionyesha kutambua uwezo wa wapinzani wao:
“Yanga ni miongoni mwa timu zenye historia kubwa zaidi nchini Tanzania. Walifika fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF hivi karibuni, na katika misimu ya hivi karibuni wamekuwa wakicheza hatua ya makundi na hata kufika robo fainali. Hii ni kazi kubwa kwetu, lakini ili ufanikiwe katika kiwango hiki lazima upimane na timu bora,” alisema Connor.
Mbinu za Kuishangaza Yanga
Kocha huyo raia wa Ireland Kaskazini aliongeza kuwa uzoefu walioupata msimu uliopita dhidi ya Simba unawapa mwanga wa jinsi ya kuikabili Yanga:
“Msimu uliopita tulicheza na Simba na tulikuwa na bahati mbaya ya kuondolewa kwa jumla ya mabao 2-1. Mchezo huu unaokuja dhidi ya Yanga, wao ndio wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda, lakini tukijituma, tukachukua nafasi zetu na kupata bahati kidogo, tunaweza kufanya maajabu na kutinga hatua ya makundi.”
Njia ya Kwenda Makundi
Mshindi wa pambano hili kati ya Yanga na Gaborone United atakutana na mshindi wa mechi kati ya CFFA (Madagascar) au Lijabatho (Lesotho) ili kuwania nafasi ya kucheza Hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga inaingia kwenye msimu huu ikiwa na kiu ya kufanya vizuri zaidi na kufika mbali zaidi barani Afrika, huku Gaborone United ikitaka kuvuka kizingiti cha timu za Tanzania baada ya kuondoshwa na Simba msimu uliopita.