USATI! Sababu ya Crystal Palace Kufanya Mazungumzo na Mchumba wa Dwight McNeil Yafichuka
LONDON, ENGLAND — Klabu ya Crystal Palace inaripotiwa kufanya mazungumzo ya faragha na Megan Sharpley, mchumba wa mshambuliaji Dwight McNeil, kabla ya kuweka saini ya mwisho kwenye dili la usajili wa nyota huyo kutoka Everton. Uhamisho huo umehusisha mabadilishano ya moja kwa moja ya wachezaji bila ada yoyote ya fedha kujumuishwa.
Usajili wa McNeil kwenda Selhurst Park ulithibitishwa rasmi baada ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 kukamilisha vipimo vyake vya afya. Katika mpango huo usio wa kawaida kwenye soka la kisasa, McNeil amejiunga na Palace huku Brennan Johnson—aliyesajiliwa na Palace miezi saba iliyopita kwa ada ya rekodi ya klabu—akielekea Everton.
Kwanini Palace Ililazimika Kumuona Mchumba wa McNeil?
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na jarida la The Times, Mwenyekiti wa Crystal Palace, Steve Parish, alilazimika kumtafuta Megan Sharpley ili kuweka mambo sawa kufuatia sakata la usajili wa mchezaji huyo kufeli mwezi Februari mwaka huu.
Katika dirisha dogo la usajili la mwezi huo, McNeil alitazamiwa kujiunga na Palace kuchukua nafasi ya Jean-Philippe Mateta aliyekuwa anahusishwa na AC Milan. Hata hivyo, baada ya Mateta kushindwa vipimo vya afya, Palace iliamua kujiondoa kwenye dili la McNeil katika dakika za mwisho, licha ya kuwa tayari walikuwa wamewasilisha nyaraka za mchakato huo Ligi Kuu Uingereza (EPL).
Hatua hiyo ilimkasirisha sana Sharpley, ambaye kupitia ukurasa wake wa Instagram alikosoa vikali usimamizi wa Palace kwa kukaa kimya na kuathiri afya ya akili ya mchezaji huyo. Sharpley alihoji kwa nini sekta ya soka inaona ni kawaida kuchezea afya ya akili ya wachezaji kwa kisingizio kuwa wanalipwa mshahara mkubwa.
Baada ya miezi sita ya mvutano huo, Steve Parish alichukua hatua ya kusafisha upepo na kumaliza tofauti hizo, hatua iliyofungua njia kwa McNeil kuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa na Crystal Palace katika dirisha hili la majira ya kiangazi.