Desiree Ellis Aweka Wazi Vita ya Banyana Banyana na Nigeria Njia ya Kombe la Dunia 2027
KOCHA mkuu wa timu ya taifa ya wanawake ya Afrika Kusini (Banyana Banyana), Desiree Ellis, amesema wanatambua ugumu na uzito wa kibarua kilichopo mbele yao wakati watakapokabiliana na miamba ya soka Afrika, Nigeria, kwenye mchezo wa mchujo wa Kombe la Mataifa ya Afrika (WAFCON).
Afrika Kusini iliondolewa katika hatua ya robo fainali baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Cameroon kwenye Uwanja wa Larbi Zaouli, Casablanca.
Miamba hiyo miwili sasa inakutana katika mechi ya “play-in” itakayopigwa Alhamisi hii kwenye Uwanja wa Moulay Rachid, Casablanca. Mshindi wa mchezo huo atakata tiketi ya kucheza mchujo wa mabara (inter-confederation play-offs) ili kuendeleza ndoto za kushiriki Kombe la Dunia la Wanawake mwaka 2027 nchini Brazil.
Licha ya presha kubwa na ugumu wa pambano hilo dhidi ya Nigeria, Ellis ameweka wazi kuwa kikosi chake hakiko tayari kupoteza nafasi hiyo ya mwisho ya kutetea nafasi ya kucheza fainali za dunia.
“Bado hatujatolewa rasmi. Tusingependa kupitia njia hii ya mchujo, lakini ndiyo hali halisi ilivyotokea na tunapaswa kuipitia. Tunachotakiwa kufanya sasa ni kujiandaa kikamilifu kisaikolojia na kimwili kwa ajili ya mechi inayofuata, huku tukihakikisha wachezaji wanapona haraka uchovu,” alisema Ellis.
Kocha huyo aliongeza kuwa anafahamu fika ukubwa wa changamoto inayowakabili, ikizingatiwa kuwa Nigeria ni miongoni mwa timu zenye historia ndefu na mafanikio makubwa katika soka la wanawake barani Afrika.
Mshindi wa pambano hili la kukata na shoka atasonga mbele kwenye mchujo wa mabara utakaozikutanisha timu 10 kutoka kote duniani, ambapo ni timu tatu tu zitakazofanya vizuri ndizo zitakazopata tiketi ya mwisho kuelekea Brazil 2027.