Selemani Mwalimu Simba na Yanga
Simba SC

Sababu za Simba Kukosa Saini ya Selemani Mwalimu na Kutua Yanga Zafichuka

Vardo August 12, 2026 10:21 am

UONGOZI wa Simba SC kupitia Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Crescentius Magori, umeweka wazi sababu zilizowafanya wajitoe kwenye mbio za kumsajili mshambuliaji Selemani Mwalimu, ambaye hatimaye ametambulishwa kama mchezaji mpya wa watani zao wa jadi, Yanga SC.

Akitolea ufafanuzi sakata hilo, Magori ameeleza kuwa mabadiliko ya ghafla ya gharama za usajili kutoka kwa klabu inayomiliki mchezaji huyo, Wydad Casablanca ya Morocco, ndiyo yaliyovuruga makubaliano ya awali kati ya Simba na klabu hiyo.

Gharama za Dili Kubadilika Ghafla

Magori amefichua kuwa Selemani Mwalimu alikuwa ameshawasili nchini na kuingia moja kwa moja kambini kwa Simba, lakini baadaye uongozi wa Wydad ulileta sharti jipya la kifedha.

“Baada ya Selemani kuwasili nchini na kuingia kambini Simba, tulipokea taarifa mpya kutoka Wydad kwamba wanahitaji kiasi cha Shilingi bilioni 1 ili kutoa mchezaji huyo kwa mkopo wa msimu mmoja pekee.

“Tulikuwa tumekubaliana kila kitu na Wydad, lakini baadaye wakabadilika baada ya kusema wamepokea ofa kubwa zaidi,” alisema Magori.

Uamuzi wa Simba Kumlinda Mchezaji na Klabu

Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa Simba haikuwa tayari kutumia kiasi hicho kikubwa cha fedha kwa ajili ya mchezaji wa mkopo wa mwaka mmoja tu, kwani kufanya hivyo kungeiletea klabu hiyo uwezekano wa kuingia kwenye mtego na changamoto za kifedha.

“Simba haiwezi kununua mchezaji kwa mkopo wa kiasi hicho. Huwezi kutoa Sh bilioni moja kwa mchezaji wa mkopo wa mwaka mmoja. Pesa ina thamani; huwezi kuwafurahisha watu kwa siku mbili halafu baadae klabu inakuja kufungiwa na FIFA,” aliongeza Magori.

Ujumbe Mzito kwa Mashabiki wa Simba

Baada ya mchezaji huyo kutambulishwa rasmi na Yanga kuelekea msimu wa 2026/27, Magori amewataka mashabiki wa Msimbazi kutokuwa na hofu wala taharuki, kwani mipango ya usajili wa nyota wengine wakubwa bado inaendelea.

“Hakuna taharuki yoyote Simba. Mashabiki wanatakiwa kutulia maana hii ndiyo Simba. Kuna mchezaji mzuri na wa kiwango cha juu anatua kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili Agosti 15, 2026. Watu watulie, Simba ni imara na itaendelea kuwa imara,” alihitimisha Magori.

Kocha wa Nigeria Justin Madugu Abeba Lawama Kichapo cha Cameroon WAFCON Simba SC Yaiva Mbadala wa Mwalimu, Kumsajili Mshambuliaji Huyu Hatari!